ESCROW MPASUKO NCHI NZIMA

TUKUBALI tukatae, sakata la fedha kiasi cha Sh. bilioni 306 zilizochotwa kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limeipasua nchi, Risasi Jumamosi limegundua.
 
Waziri mkuu Mizengo Pinda.
Escrow imeipasua nchi kufuatia majadiliano ya waheshimiwa wengi kuanzia juzi, Alhamisi kuonekana kila mmoja ana upande wake huku wapiga kura wao nao wakiwa kinyume na wawakilishi hao.Risasi Jumamosi liligundua kuwa, mara tu baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujitetea kufuatia uchunguzi wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kumtia hatiani kuhusika na uchotwaji wa fedha hizo, mitandao ya kijamii ilianza kugawanyika. Mitandao hiyo, tofauti na ilivyokuwa kabla ya Waziri Muhongo hajajitetea ambapo ilikuwa ikisisitiza aachie ngazi, ilianza kumtetea na kusema Kamati ya Zitto iliumbuka ikidai mheshmiwa huyo alijitetea vizuri kwa kuanika ukweli wenye ushahidi. Katika uchangiaji wa hoja kwenye mitandao, wengine waliwapinga wanaomtetea Muhongo wakidai walipewa ‘kitu kidogo’.
Hata hivyo, katika mjadala wa bunge hilo jioni ya juzi, mchangiaji wa kwanza, mheshimiwa Tundu Lissu alipopewa nafasi na kupingana na utetezi wa Profesa Muhongo, mitandao ya kijamii nayo ikagawanyika tena ambapo wengi walisema Lissu alikuwa na hoja.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili juzi jijini Dar kila mmoja alionekana kuwa na maelezo yanayopingana na upande mwingine. “Mimi nakubali waliotajwa wote kwenye Kamati ya PAC waachie ngazi, maana wamekula kweli yale mabilioni ya Escrow,” alisema Julius Sempinda, mkazi wa Kimara, Dar.
Sempinda wakati akisema hayo alikuwa na nduguye aliyemtaja kwa jina la Joseph Sempinda ambaye aliwatetea wote waliotuhumiwa na kamati ya Pinda na kusema fedha za Escrow si za umma wala za serikali.
“Wabongo ni wivu tu unawasumbua. Zile bilioni 306 si za serikali wala za umma. Pesa ni halali kulipwa kwa IPTL,” alisema Joseph.
Kwenye vyombo vya usafiri wa umma juzi, mazungumzo yalikuwa hayo, kwamba  Escrow ni fedha ya umma au la! Mijadala ndani ya vyombo hivyo ilikuwa haiishi kwa sababu kila upande ulikuwa na mtazamo wake.
Ili kuonesha kuwa Escrow imepasua nchi, wako waliokuwa hawapo upande wowote katika kutetea au kupinga. Sakata la Escrow limemgusa Waziri Muhongo, naibu wake, Steven Masele, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi. Wengine ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadhi ya watumishi wa serikali kutoka Benki Kuu, Rita na TRA. Kamati ya PAC ikitumia ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliwataka watumishi hao wa serikali kuwajibika mara moja.

Post a Comment

Previous Post Next Post