Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
jana alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
kuhusu ufisadi uliofanyika katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuacha
wananchi njia panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli kati yake na
kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti
yake kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo amekuwa mara kwa mara
akilipotosha Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo
hakukuwa na fedha za umma.
Kamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa
Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Singh Sethi na
James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine hilo ndilo
lilikuwa sababu ya upotoshaji.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo,
Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine ingawa
katika mjadala wa baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine waliohoji
uhalali wa vielelezo alivyotoa.
Kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC
kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa kuwa kulingana na mkataba
wa PPA kati ya Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga,
kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha
mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa Mei 26, 1995.
“Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza
Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye
Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya
uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji.”
Gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka 2004
Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa
Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya
gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema suala hilo si kweli.
Alifafanua kuwa Tanesco haijawahi kufungua shauri
lolote ICSID ya London au Mahakama yoyote dhidi ya Benki ya Standard
Charterd kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa na
PAC.
“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010
na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya
deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya
Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na
Tanesco na wala siyo Tanesco na IPTL.”
Alisema Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana
na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo
ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo
kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na mkataba wa
kibiashara baina yao.
- Soma Zaidi Hapa(Mwananchi)
- Soma Zaidi Hapa(Mwananchi)
إرسال تعليق