ESCROW
kila kona! Wabongo wameibuka na msemo mpya kuhusu sakata la uchotwaji
wa fedha za umma kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), wakilitolea tafsiri iliyobeba kichwa cha habari
hii kwamba Escrow ni Eneza Siasa Chota Riziki Ondoa Woga.
Waziri mkuu Mizengi Pinda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wananchi
wamesema mtu akitaka riziki kirahisi ajiingize katika siasa na kuanza
kuihubiri pia aondoe woga kama washiriki katika sakata hilo walivyofanya
kwa kujipa ujasiri wa kujichotea shilingi bilioni 306 kutoka kwenye
akaunti hiyo.
ISIKIE HII“Sasa nimeamini, ukitaka kuwa tajiri mkubwa katika nchi hii, we eneza siasa, utaweza kuchota riziki (pesa) kubwa sana hususan kama utaondoa woga,” alisema Fred Jimmy ‘Fredwaa’, mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam. Pamoja na yote hayo, wananchi hao wamesema chochote kitakachofanyika, ni lazima fedha hizo zirejeshwe kutoka kwa wahusika hao, kwani ni fedha za walipa kodi wa Tanzania ambao maisha yao ya kila siku ni ya kubangaiza.
Askofu Mkuu Msaidizi Jimbo la Kagera, Methodius Kilaini.
“Ripoti ya PAC tumeiona na utetezi wa Waziri Sospeter Muhongo pia
tumeusikia, lakini hatuukubali. Anadai kuwa Tanesco haina fedha kwa kuwa
haijaanza kutengeneza faida, kwamba kwa muda wote imekuwa ikidaiwa tu.
“Sawa, hatukatai Tanesco inadaiwa (bilioni 90 na capacity charge’)
lakini si ni kweli pia kwamba Tanesco hiyohiyo ilikuwa inaweka yale
mabilioni kwenye ile akaunti ya Escrow?” alihoji mwananchi mmoja
aliyejitambulisha kama Justin Sompa, mfanyakazi serikalini jijini Dar es
Salaam.
Akaendelea: “Kwa hiyo kwa akili ya kawaida, madeni yanayodaiwa
Tanesco hayana uhusiano na fedha za Escrow na ukweli unabaki kuwa kwenye
Kamati ya Zitto (PAC), hizi pesa zinatakiwa zirudi mara moja na
waliohusika lazima wapandishwe kizimbani na ikibidi wafilisiwe mali
zao.”
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
WATU WAFANYA BONGE LA SHEREHEWakati gazeti hili linakwenda mitamboni jana, kuna habari kuwa, baadhi ya watu jijini Dar na Dodoma kutoka kwenye makundi ya urais 2015 ambao hawakujulikana kambi, walikesha juzi wakila na kunywa kufurahia anguko la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye mbio hizo. “Kashfa hii kwa Pinda ni anguko kwa uchaguzi wa urais mwakani. Ripoti ya Twaweza ilimtaja kushika nafasi ya pili baada ya Edward Lowassa, sasa kachafuka ni dhahiri ameshuka kisiasa.
“Unadhani kwa muda uliobaki kufika mwakani atatumia mbinu gani ili atakate kama zamani?” alihoji mmoja wa watu wa kambi hizo. Watu hao walifurahia zaidi kwa kudai kuwa, kama ni uwanjani Pinda alikuwa akipiga mpira wa penalti ambao ameutoa nje ya uwanja na kuliacha goli (angalia mchoro ukurasa wa kwanza). WAKATOLIKI WAMBANA KILAINI
Wakati huohuo, baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania wamemtaka Askofu Mkuu Msaidizi Jimbo la Kagera, Methodius Kilaini kujieleza alipewa kitita cha shilingi milioni 80 na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabibo Bier, James Rugemalila kwa ajili ya kitu gani?
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Hata hivyo, mtu mmoja alilipenyezea Ijumaa jana kuwa, Rugemalila na
Kilaini ni marafiki waliosoma pamoja japokuwa bado urafiki huo
haujitoshelezi kupeana kiasi hicho cha pesa.
MWANASHERIA MKUUAidha, wananchi wamemtaka pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kuachia ngazi na baadaye mamlaka zimpeleke mahakamani kwa kuisababishia hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 20 kama kodi, baada ya kusema uongo kuwa fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo, hazikutakiwa kukatwa kodi ya ongezeko la thamani wala mhuri wa stempu. “Huyu alitoa kauli ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) waliotaka kukata kodi, lakini pia aliidanganya Wizara ya Fedha kwa kusema fedha hizo ni za IPTL wakati anajua kabisa kuwa ni za umma. Kwa kiongozi mkubwa wa serikali kama huyu, anapodanganya na kuisababishia hasara nchi, ni mtu wa hatari sana, hafai kukalia kiti kile, amepoteza sifa,” alisema mwanafunzi mmoja wa mwaka wa pili wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina moja la Daffa.
William Ngeleja.
“Huyu anaonesha jinsi serikali yetu ilivyo na watendaji waliooza,
yupo tayari mamilioni ya wananchi wateseke ili mradi tu ashibishe tumbo
lake na familia yake. Kwa cheo chake anapata fedha na marupurupu mengi,
lakini haridhiki, nchi inatafunwa sisi tumekaa tunaangalia, tunaona kama
haituhusu, tuamke jamani,” alisema Daffa akionekana kuwa na uchungu
mwingi.
BOSI WA IPTLMtu mwingine aliyetajwa kuwa anastahili kufikishwa katika vyombo vya sheria, ni pamoja na mmiliki wa kampuni ya IPTL, Singh Harbinder Sethi ambaye licha ya ukweli kwamba alistahili sehemu ya fedha hizo, lakini kitendo chake cha kuwasilisha nyaraka za kugushi, akiidanganya serikali kuhusu manunuzi ya hisa zake na hivyo kukwepa kodi halali, ni kosa la jinai. “Kamati ya PAC imeonyesha jinsi alivyokuwa akiidanganya serikali (TRA) kuwa ameuza hisa kwa fedha kidogo wakati ameuza kwa bei kubwa, haiwezekani tuwachekee hawa watu wakati sisi wananchi wetu wanakufa kwa kukosa dawa mahospitalini halafu fedha zetu zinaibiwa kirahisi tu,” alisema Daffa.
Jaji Werema.
Wengine waliotajwa kuhusika na fedha zilizochotwa na ambao pia
wanatakiwa kufikishwa mahakamani ni pamoja na Andrew Chenge, mwanasheria
mkuu wa zamani, Waziri wa Nishati na Madini wa zamani, William Ngeleja
na Mkurugenzi wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Fedha za Escrow zitapazo shilingi bilioni 306 zilichukuliwa katika
akaunti hiyo na kwa mara ya kwanza, liliibuliwa bungeni na mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye hata hivyo, alishambuliwa na
watendaji mbalimbali wa serikali, kwa kuitwa mwongo.
Miongoni mwa waliosakama ni pamona na Mwanasheria Mkuu Jaji Werema
ambaye alifikia hatua ya kumuita Tumbili. Pia Waziri wa Nishati na
Madini, Sospeter Muhongo (Pichani), Naibu wake Steven Masele na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
إرسال تعليق