Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akikazia hoja.
YATOKANAYO na sakata la uchotwaji wa fedha kwenye
akaunti maalum ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni
mengi, lakini kubwa ni kuvuliwa nguo kwa utawala wa nchi. Akichangia
bungeni hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema
mambo ya Escrow yalipaswa yafanyike kwenye nchi zisizokuwa na udhibiti
wa dola, akitolea mfano Kongo na Somalia.Katika hali ya kawaida yalikuwa ni maneno machache lakini mazito, sina hakika kama viongozi wa juu wa serikali walimwelewa alichomaanisha, pengine ndiyo maana sura zao hazikuonesha aibu juu ya kauli hiyo.
Lakini wenye kufikiri; matamshi hayo hayakuwa na sura njema kwa rais, waziri mkuu, mawaziri pamoja watendaji wa serikali vikiwemo vyombo vinavyosimamia usalama wa nchi.
Sarakasi za uchotwaji wa shilingi bilioni 306 katika akaunti ya Escrow zimepita kawaida na kusema kweli zinastaajabisha na kuogopesha mno.
Kwamba ‘wahuni’ wachache wanaweza kubuni uongo na kuielekeza BoT ambayo ni taasisi nyeti ya fedha za nchi itoe kiasi hicho kikubwa cha fedha bila vyombo vya usalama na watalawa kujua kinachoendelea, bila shaka alichokisema Zitto hakipingiki.
Kwa kukubaliana na hilo; nimeamua kuyapa makala haya kichwa cha habari hapo juu kwa mantiki kuwa hata kama viongozi wa ngazi za juu hawakuhusika moja kwa moja na sakata hilo bado hawawezi kukwepa udhaifu wa utawala wao.
Ikiwa vyombo vya usalama vilishindwa kubaini uchotwaji wa fedha nyingi kiasi hicho na kuwaacha watu wachache wakizifanyia mgawo ndani ya nchi wanayoiongoza, itakuwaje kwenye udhibiti wa fedha za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri; watu si watajichotea watakavyo?
Ndiyo maana nimesema, viongozi ndani ya serikali wawajibikie kwanza udhaifu wao, watubu mbele ya umma kuwa wameshindwa kwa kiasi kikubwa kulinda mali za wananchi, baada ya hapo zamu ya wezi wa fedha za Escrow iwadie na wote waliohusika wapelekwe msalabani.
Kama njia hii ya uwajibikaji ikishindikana, udhaifu utaendelea kuwapa fursa wezi wa mali za wananchi na kila siku tutakuwa na wimbo mpya wa ufisadi, mara EPA, Richmond, Escrow na kadhalika zake.
Naandika makala haya katika sura hii si kama sielewi upande wa pili wa shilingi, la! Nimesikia hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda naye anahusika katika sakata hili huku mtu anayeitwa ‘Bwana Mkubwa’ naye ametajwa kuujua mchezo.
Hili sikulipa kipaumbele sana kwa sababu watuhumiwa wanatumia nguvu kubwa sana kujinasua; wameulizwa mara kadhaa wamejitetea kuwa hawahusiki, lakini kutokuhusika kwa waziri mkuu kuna maana gani kama fedha nyingi kiasi hicho zimechotwa na yeye akiwa mwenye dhamana?
Kutohusika kwa rais wa nchi kuna maana gani kama bilioni 306 zimeibwa na wajanja wakati yeye akiwa na dhamana ya wananchi waliomchagua awaongoze na kuwalinda? Hapa ndipo niliposimamia, sitaki kuhukumu juu ya wizi nisiokuwa na ushahidi nao.
Narudia kusema; viongozi wa serikali, wameiba au hawajaiba wana jukumu la kuutubia udhaifu wao mbele ya wananchi kwa kushindwa kwao kujua njama za wizi mkubwa wa mali za umma.
Hili peke yake katika nchi zinazojali uwajibikaji, lilitosha kabisa kuwaondolea sifa baadhi ya watendaji na kuwapotezea sifa za uongozi bila kusubiri ushahidi wa kuhusika kwao moja kwa moja na wizi.
Nachochea tu!
إرسال تعليق