WAKATI
fomu za kugombea ujumbe wa Serikali za Mitaa zikianza kutolewa rasmi
jana, zimelalamikiwa na vyama vya siasa kwamba maelezo yake
yanatatanisha hususani kifungu cha 21 na 22, ambako mgombea anatakiwa
kujaza nembo ya chama chake na halmashauri.
Suala hilo, liliwahi kulalamikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe, wakati akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi
hivi karibuni, akisema kuwa wamebaini kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kinataka kutumia mbinu hiyo kuwaengua wagombea wa upinzani
watakaoshindwa kutimiza matakwa ya vifungu hivyo.
Kwa mujibu wa fomu hiyo ambayo Tanzania Daima limeona nakala yake,
mgombea anatakiwa kujaza nembo ya chama chake na halmashauri bila
kufafanua anatakiwa kuzitaja alama zilizopo kwenye nembo hizo ama
kuzichora, suala ambalo limeibua utata mkubwa kwa wagombea.
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa CHADEMA, John Mrema,
alizungumzia utata huo kuwa ni mbinu chafu iliyoandaliwa kwa makusudi
ili kuvuruga uchaguzi huo, jambo alilosema hawako tayari kwa hilo.
“Jambo hili tulimwandikia barua rasmi Waziri Mkuu na mpaka leo mwezi
mmoja umeishia hakuwahi kulitolea ufafanuzi wowote, achilia mbali kujibu
barua yetu tuliyomuandikia kutaka ufafanuzi huo na hata alipotoa
mwongozo wa uchaguzi huu, hakulizungumzia hata kidogo.
“Ukisoma fomu zilizoanza kutolewa leo SEHEMU A: Maelezo ya Mgombea,
utaona kuwa kifungu cha 21 na 22 ndivyo vinamtaka mgombea kujaza nembo
ya chama chake na ya halmashauri yake,” alisema.
Mrema, alifafanua kuwa jambo hilo limewachanganya sana wanachama wao
hasa kitendo cha kumtaka mgombea ajaze nembo ya halmashauri na ya chama
chake, kwamba ikumbukwe kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), amenunuliwa na magazeti akisema kuwa
wanasiasa wanaozungumzia suala la nembo ni porojo na hakuna kitu kama
hicho.
“Kabla hata ya wino ulioandika maneno yake haujakauka ametoa fomu
ambazo zinataka mgombea kujaza nembo ya chama na ya halmashauri, hizi ni
dalili za wazi kuwa serikali hii imefikia ukomo wa kufikiri na haipo
makini hata kidogo, inayumba na imepoteza mwelekeo,” alisema Mrema.
Alisisitiza kuwa, wanataka Tamisemi watoe ufafanuzi wa kina kuhusu
fomu hizo kama ni halali kwa mgombea kutakiwa kujaza nembo ya
halmashauri na ya chama chake, kwamba ijulikane wazi kuwa kuchora nembo
hizi ni kazi ngumu sana, kwani nyingine ni vigumu kuzichora.
“Tunataka waeleze kama ni halali kwa mgombea atakayeshindwa kujaza
fomu hizi itakuwa kigezo kimojawapo cha kuwekewa pingamizi na hatimaye
kuenguliwa kwenye uchaguzi husika, kwani ikiachwa kama ilivyo
inasababisha vurugu katika uchaguzi huu,” alisema Mrema.
- Tanzania Daima
إرسال تعليق