HAJA NDOGO MRIJA WAKE, HAJA KUBWA MRIJA WAKE

Stori:   makongoro oging’
“Maishi yangu yako hatarini, nachungulia kaburi, nimeteseka kwa muda mrefu bila kupona wala msaada, nimetoka katika ukoo maskini unaotegemea kwa asilimia kubwa kilimo cha jembe la mkono, nitapata wapi shilingi milioni moja na laki tano na arobaini na tano elfu ili nikatibiwe?”
Hii ni sehemu ya kilio cha Steven John anayesumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya tumbo.

Steven John anayesumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya tumbo.
AMETOKA WAPI?
John ni mkazi wa Kijiji cha Sokoni One, mkoani Arusha, amekua akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa kipindi cha miaka miwili bila kupata nafuu na hali yake inazidi kubadilika kila mara ingawa ametakiwa na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kufanyiwa upasuaji wa pili baada kufanyiwa hivyo huko nyuma.
Mgonjwa huyu anazunguka huku na kule kutafuta fedha bila mafanikio na kwa sasa anawaomba watu wenye huruma wamchangie ili akamilishe tiba yake.

FAMILIA INAISHIJE?
“Nina familia ya mke na watoto nane, walikuwa wakiishi kwa kunitegemea lakini kwa kipindi cha miaka miwili sasa wamekosa msaada wangu, kwani nimekuwa nikizunguka hospitali kadhaa huku nikiwa na mke wangu kutafuta matibabu lakini tunakumbana na vikwazo vingi kikiwemo cha ukosefu wa fedha.

“Jambo hilo linanifanya niwe na mawazo mengi sana ya kumtaka Mola aichukue roho yangu, kwani nimeanza kuchungulia kaburi kuliko kuisumbua familia yangu inayoteseka kwa kukosa matunzo nami kuteseka kwa maumivu makali, nimekuwa ombaomba hapa mjini ili nipate fedha lakini hakuna mafanikio.
Muonekano wa sehemu za kutolea haja kubwa na ndogo.
UGONJWA ULIANZAJE?
“Nakumbuka ugonjwa huu ulinianza Oktoba mwaka juzi, ulianza kwa tumbo kuunguruma pia nilipoteza hamu ya kula hali iliyonifanya niende katika zahanati ya kijijini kwetu, wao walinieleza kwamba nina vidonda vya tumbo walinipa dawa nikapata nafuu kidogo lakini baada ya muda hali ilibadilika na kuwa mbaya.

“Ikatokea kwa siku kumi na saba sikwenda haja kubwa, tumbo lilivimba kiasi cha kutaka kupasuka, nikaenda Hospitali ya Mount Meru, Arusha, nilifanyiwa vipimo kikiwemo cha x-ray, wakagundua kuwa sehemu ya haja kubwa kumeziba ikabidi wanifanyie upasuaji, pia walitoboa tumbo nikawa najisaidia kwa kutumia mpira.
“Baada ya siku mbili tangu nifanyiwe upasuaji huo, kibofu cha mkojo kikawa kinauma baada ya mrija kuziba, nilifanyiwa upasuaji nikawa najisaidia kwa kutumia mpira baada ya tumbo kutobolewa tena, huu mfuko wa kulia ni wa haja ndogo na wa kushoto ni wa haja kubwa.
AKATWA KIPANDE CHA NYAMA
“Nikiwa bado nipo Mount Meru madaktari walikata kipande cha nyama pajani na kukipeleka Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa vipimo na majibu yalipokuja iligundulika kuwa nina saratani ya utumbo mpana.
“Walinieleza nije hapa Dar, Hospitali ya Ocean Road ambapo niliendelea na matibabu, ilipofika Septemba 16, mwaka huu nilishauriwa niende Muhimbili nikafanyiwe vipimo kama saratani imeisha.

“Lengo lilikuwa kama ugonjwa hakuna, niweze kurejeshewa mfumo wa haja kubwa na ndogo katika hali ya kawaida. Hata hivyo, nilipofika Muhimbili nilifanyiwa kipimo kimoja cha City Scan na vingine bado, ndiyo maana nahangaika kutafuta fedha ili nikakamilishiwe vipimo hivyo kisha nifanyiwe upasuaji mwingine.
“Kwa kuwa sina fedha, nawaomba wasamaria wema wanisaidie ili nifanyiwe vipimo na upasuaji mwingine, sina raha hapa nilipo. Napatikana kwa simu namba 0712 820440 au 0752 225061,” alisema John kwa huzuni.

Post a Comment

أحدث أقدم