Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mbunge wa
Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kusema amelishwa sumu akiwa London,
Uingereza, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amemtaka kusema ukweli
na si kulihadaa Taifa kwa uongo.
Mkono akizungumza na waandishi wa habari juzi
kuelezea mwenendo wa afya yake, alisema lengo la kulishwa sumu ilikuwa
ni kutaka kuharibu figo zake ndani ya saa 72 kitendo kilichoshindikana.
Mdee aliyekuwa na Mkono katika ziara hiyo alisema:
“Hakuna ukweli wowote kwamba alilishwa sumu, nilikuwa naye kule na
mazingira aliyoanza kuumwa hadi kupona kwake ni utata... awaeleze
Watanzania anaumwa nini na si kusema alilishwa sumu.
“Nilikaa kimya baada ya kuripotiwa na gazeti moja
(The Citizen) kwamba Mkono kalishwa sumu, sasa amezungumza tena nikaona
si busara kukaa kimya wakati alilidanganya Taifa. Mkono waeleze ukweli
watu mbona unawadanganya.”
Mdee aliwataja baadhi ya wajumbe wa msafara huo wa
watu 11 kuwa ni William Ngeleja (Mwenyekiti wa kamati hiyo), Mkurugenzi
wa Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk Edward Hoseah,
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala
Bora), George Mkuchika.
“Dk Hoseah ndiye aliyezungumza na daktari wa Mkono
kwa kina zaidi na alimweleza kuwa ampatie dawa fulani, sasa kama kweli
alilishwa sumu daktari wake alijuaje kuwa sumu hiyo inaondolewa na dawa
hiyo aliyomwambia Hoseah ampe.
“Kama ni kutaka kutumia kivuli cha sakata la
escrow, arudi bungeni tuijadili na tuimalize ila asiseme kuwa sijui
wanataka kumuua ni uongo,” alisema Mdee.
Kuhusu vitisho alivyodai Mkono kutumiwa kabla ya
safari hiyo, Mdee alisema: “Kama kweli ni vitisho iweje tulivyokwenda
aliamua kulala peke yake, wewe upo safarini na wenzako halafu ukatishwa
kuuawa utakwenda kulala peke yako au utalala na wenzako?”
Mkono alisema anaendelea vizuri na anasubiri kujua hatima ya uchunguzi unaoendelea ili kubaini chanzo cha kulishwa sumu.
“Niko vizuri na afya njema... kama kuna mtu
anawinda jimbo langu, mwambieni ameshindwa na wananchi wangu nawaeleza
kuwa niko salama wasiwe na hofu. Ninataka kujua nani kanilisha sumu na
kwa nini?
“Tukiwa uwanja wa ndege nilipokea ujumbe mfupi wa
maandishi (hakutaka kuuweka wazi kwa sababu upelelezi haujakamilika),
ukinitahadharisha kuwa makini, ujumbe ule ulinishtua kwa kweli,”alisema- Mwananchi
Post a Comment