WIZARA
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeendeleza msimamo wake kuwa Tanzania bado
haina sheria ya kuwaruhusu wafungwa kukutana kifaragha na waume au wake
zao.
Hii ni mara ya tatu kwa serikali kutoa majibu hayo kutoakana na
maswali ya wabunge, ambako mara kadhaa swali hilo limekuwa likiulizwa na
Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Msabaha (CHADEMA).
Jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima,
alikiri kuwa Tanzania haina sheria hiyo na akajibu kuwa, ujauzito ambao
huwapata wafungwa wanawake, unatokana na kuupata nje ya magereza.
Alitoa majibu hayo kutokana na swali la Mbunge wa Viti maalum, Rukia
Kassim Ahmed (Cuf), ambaye alitaka kujua ni kwa namna gani wafungwa
wanawake wanapata ujauzito wanapokuwa ndani ya magereza yao.
Mbunge huyo, pia alihoji kama magerezani kuna usiri, ni kwa namna
gani mahabusi ambao ni mashehe kutoka Zanzibar wanafanyiwa vitendo vya
ulawiti gerezani.
Naibu Waziri huyo, alisema kuwa Jeshi la Magereza lina utaratibu wa
kutenganisha wafungwa wa kiume na wa kike, kwani kila watu hutunzwa kwa
sehemu zao na hulindwa na watu wa jinsia zao.
Kuhusu tuhuma za kulawitiwa kwa Mashehe wa Zanzibar, Waziri wa Mambo
ya Ndani Mathias Chikawe, alisema kuwa sakata la Sheikh Salum Ali
Salumu, linafanyiwa kazi na kwamba kiongozi huyo ameshafanyiwa uchunguzi
wa awali katika hospitali ya Amana.
“Jambo hilo lipo mikononi mwetu, tumempeleka hospitali ya Amana na
kesho (leo) tutampeleka hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi,
lakini tunachunguza pia tabia ya kiongozi huyo na mwenendo wake kabla ya
kuingia gerezani,” alisema Chikawe.
Hata hivyo, Chikawe alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa
watuhumiwa hao, kwani tangu mwanzo hakuwa ameripoti vitendo hivyo lakini
alipofika mara ya nne gerezani ndipo akaripoti kufanyiwa vitendo hivyo
na mmoja wa askari polisi.
إرسال تعليق