Katuni
Uthibitisho huo ulijionyesha jana baada ya Bunge kuamua kuendelea na shughuli zake, hususan, kuwasilishwa na kujadili hoja ya mgogoro wa uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ni matokeo ya mgogoro wa ulipaji wa gharama za umeme uliokuwa unauziwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mkataba huu ulifungwa Mei 26, 1995, kati ya Tanesco na IPTL. Makubaliano hayo yalitakiwa yadumu kwa miaka 20. Yaani yangehitimishwa mwaka ujao, 2015. Haya yalilenga Tanesco kununua umeme kutoka IPTL uliokuwa unazalishwa na mitambo yake iliyoko Tegeta, Dar es Salaam.
Yaligawanyika katika sehemu mbili; mosi, malipo ya manunuzi ya umeme (Energy Purchase Price) na pili, malipo ya kiwango cha uwekezaji (Capacity Purchase Price au Capacity Charge.)
Baada ya moto kuwashwa bungeni huku umma ukisubiri taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuchambuliwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wapo watu waliokimbilia mahakamani ili kuwaziba midomo wabunge na Bunge kwa ujumla ili wasijadili sakata hili ambalo limetikisa sana taifa kwa kipindi cha miezi zaidi ya sita sasa.
Jana Spika wa Bunge Anne Makinda, alisema wazi kwamba kwa mujibu wa sheria za nchi hii, Bunge haliwezi kupelekewa samansi yoyote (hati ya kimahakama) na mtu yeyote au mamlaka yoyote wakati likiendelea na shughuli zake, kwa maana hiyo kazi ya kupokea, kujadili ripoti ya sakata la Tegeta Escrow akaunti ingeendelea na kweli iliendelea jana.
Maamuzi haya ya Bunge kuendelea na shughuli zake, yanafurahisha na kwa kweli kujenga na kuweka misingi imara dhana ya mgawanyo wa madaraka ya dola baina ya mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Bunge, Mahakama na Serikali (Executive). Ni hali ambayo inapaswa kuigwa na kuenziwa.
Jana Makinda alisema kwamba jambo lililotokea juu ya maamuzi ya mahakama kuagiza Bunge jambo la kufanya, ni historia kwa Tanzania kwani tangu taifa hili lipate uhuru mwaka 1961 haijapata kutokea kwa mihimili miwili ya dola kuingia katika aina yoyote ya msuguano. Hata hivyo, Spika aliwaasa wabunge kuwa na staha na kuheshimu uhuru na hadhi ya mahakama wakati wa mjadala huo.
Tukio hili siyo la kawaida, tangu wiki iliyopita habari zilipovuma kwamba kulikuwa na njama za baadhi ya watu kuitumia mahakama kulinyamazisha Bunge, nchi imekuwa kwenye hali ya wasiwasi mkubwa. Hali hii imewafanya wengi waamini kwamba taifa lilikuwa linaingia kwenye mgongano mkubwa wa kimhimili.
Kwa miaka kadhaa sasa taifa hili limekuwa linakumbwa na kashfa kubwa kubwa za uchotaji wa fedha za umma; fedha hizo zimejengea wakwapuaji wake kiburi na jeuri kiasi cha kuanza kutisha taifa hili na hata kuanza kujenga mazingira ya kugonganisha mihimili ya dola.
Ni hali inayostahili kupigwa vita.
Kama Bunge lilivyothibitisha jana, kashfa ya Escrow imechafua hali ya hewa nchini, imeonyesha jinsi fedha inavyoweza kutumika kukengeusha sheria, kurubuni watu, kuvuruga uchumi na hata kuibua uwezekano wa mgogoro wa kiutawala katika nchi kama ambavyo waliokimbilia mahakamani walitaka iwe kwa kugonganisha Bunge na Mahakama kama mihimili ya madaraka ya dola inayojitegemea.
Tunafarijika kwamba pengine kilichotokea bungeni jana na kwa msimamo ambao umeonyeshwa na muhimili huo, sasa tunaweza kusema kuwa serikali na watendaji wake wakati wote ni lazima sasa wajue kwamba wanakalia ofisi za umma kama dhamana. Ni lazima wajue kuwa wanapofanya maamuzi yoyote ni lazima wafuate sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika.
Viongozi wa serikali watambue kwamba Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, lina mamlaka ya kusimamia na kuishauri serikali. Watu sasa wajue kuwa kiburi cha madaraka na fedha asilani haviwezi kuipora nguvu na mamlaka ya wananchi ambayo yamekasimiwa kwa Bunge.
Tunafurahi kwamba kwa mara nyingine tena Bunge limesimama kama muhimili imara wa madaraka ya dola, limetaka kuwajibishwa kwa wote waliohusika katika kashfa ya Tegeta Escrow bila kubagua, wakubwa kwa wadogo kwa nia moja tu, kuhimiza uwajibikaji, nidhamu na uadilifu kwa utumishi wa umma.
Pengine hatua na msimamo huu wa Bunge utasaidia kuirejesha serikali katika mstari na kwa maana hiyo kuwafanya watendaji wake kujikita katika misingi ya utawala bora. Tunapongeza msimamo na hatua ya Bunge kwa na wivu na madaraka yake ili kutekeleza wajibu wake muhimu wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق