Dodoma. Bunge limehitimisha mjadala wa Kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow kwa kupitisha maazimio manane, likiwamo la
kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine waliowajibishwa pamoja na mawaziri hao ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kuwavua nyazifa zao
wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge.
Wenyeviti waliovuliwa nyadhifa zao ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.
Viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao chini ya azimio la Bunge namba
mbili.
Maazimio hayo mapya manane yalisomwa bungeni jana
jioni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe.
Akizungumza bungeni Zitto alisema, mabilioni ya
fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow yametumika kuwapa
kile kinachoonekana kuwa ni rushwa.
Zitto alisema baadhi ya watu waliochukua fedha
hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa Serikali kama mawaziri, majaji,
wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma,
viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria
uzembe na makosa mbalimbali ya jinai kama vile wizi, ubadhilifu
kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea
mali ya wizi,” alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge ni kulitaka
Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue
hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na taarifa
maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na
miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia
uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo hivyo vya
jinai, watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka Kamati husika za kudumu
za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano
wa 18 wa Bunge kuwavua nyazifa zao za wenyeviti wa kamati husika za
Bunge. Zitto alitaja azimio la nne ni la kumuomba Rais auende Tume ya
kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius
Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alisema utaratibu wa kushughulikia nidhamu za
majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya
Kijaji, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
Pia azimio la tano ni mamlaka husika za kifedha na
za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya
Escrow, kuwa taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment