Wasomi, wananchi walipongeza Bunge

Dar es Salaam. Wasomi, wanasiasa na wananchi wamepongeza mapendekezo mapya ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) yanayoazimia kuwawajibisha wale wote waliohusika na kuchotwa kwa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akisoma mapendekezo manane yaliyokubaliwa na pande tatu ya PAC, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Serikali, alisema kila aliyehusika katika sakata hilo atachukuliwa hatua.
Miongoni mwa watakaohusika na azimio hilo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambao imependekezwa kwa mamlaka husika kutengua uteuzi wao.
Wakizungumzia uamuzi huo walisema, kilichofanywa na Bunge hilo kinatakiwa kuungwa mkono, lakini wakatahadharisha mamlaka ya uteuzi itekeleze maadhimio ya Bunge.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Prinus Saidia alisema uamuzi uliofikiwa na Bunge ni mzuri ambao unaleta imani kwa wananchi waliokuwa wakifuatilia mjadala huo.
“Ingekuwa jambo la busara hawa waliotuhumiwa wangewajibika mapema na siyo kusubiri hadi Bunge lilipofikia,hii ni hulka ya viongozi wa Afrika kutopenda kuwajibika hata kama ikibainika walifanya makosa, ” alisema.
Alisema fedha hizo zinatakiwa kuhakikisha zinarudi na zielekezwe kulipa madeni katika bohari ya dawa, kununua vifaa tiba na kuboresha sekta nzima ya afya kwa manufaa ya Watanzania walio wengi.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema kwa hali ilivyo haoni kama kuna tatizo lolote kwa Bunge kuchukua uamuzi huo. Alisema Kamati ya PAC na Bunge walifanya kazi nzuri kwa kurejea ripoti za CAG, Takukuru kuwa fedha hizo ni za umma, hivyo kilichofanywa na Bunge kwa wahusika ni sahihi.
“Tanesco ni shirika la umma, kama wanadaiwa inakuwa ni Watanzania ndiyo wanadaiwa, kama wana fedha nyingi ni za Watanzania, kama hawana fedha ni Watanzania hawana fedha, hivyo hakuna haja ya kubishana kuwa fedha ni za nani kwa kuwa shirika hilo ni la umma,” alisema Profesa Moshi.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Cathleen Sekwao alisema, “Bunge limemaliza kazi yake kilichobaki ni utekelezaji wa maazimio.”
“Bado sijajua kwa nini zile fedha Sh73 bilioni ambazo wanasema zilipitia Benki ya Stanbic hawakutajwa wahusika nao wanatakiwa kutajwa ili Watanzania wawajue.”
Aliongeza; “Kila siku tunalalamika hakuna madawati, vyumba vya madarasa, mishahara ya walimu na maabara sasa fedha hizo Rais Jakaya Kikwete ahakikishe zinarudi ili zikatatue changamoto hizi ambazo ni tatizo.”
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post