Dar es Salaam. Wasomi, wanasiasa na wananchi
wamepongeza mapendekezo mapya ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) yanayoazimia kuwawajibisha wale wote waliohusika na kuchotwa kwa
fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akisoma mapendekezo
manane yaliyokubaliwa na pande tatu ya PAC, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni na Serikali, alisema kila aliyehusika katika sakata hilo
atachukuliwa hatua.
Miongoni mwa watakaohusika na azimio hilo ni
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu
wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema ambao imependekezwa kwa mamlaka husika kutengua uteuzi wao.
Wakizungumzia uamuzi huo walisema, kilichofanywa
na Bunge hilo kinatakiwa kuungwa mkono, lakini wakatahadharisha mamlaka
ya uteuzi itekeleze maadhimio ya Bunge.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk
Prinus Saidia alisema uamuzi uliofikiwa na Bunge ni mzuri ambao unaleta
imani kwa wananchi waliokuwa wakifuatilia mjadala huo.
“Ingekuwa jambo la busara hawa waliotuhumiwa
wangewajibika mapema na siyo kusubiri hadi Bunge lilipofikia,hii ni
hulka ya viongozi wa Afrika kutopenda kuwajibika hata kama ikibainika
walifanya makosa, ” alisema.
Alisema fedha hizo zinatakiwa kuhakikisha zinarudi
na zielekezwe kulipa madeni katika bohari ya dawa, kununua vifaa tiba
na kuboresha sekta nzima ya afya kwa manufaa ya Watanzania walio wengi.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey
Moshi alisema kwa hali ilivyo haoni kama kuna tatizo lolote kwa Bunge
kuchukua uamuzi huo. Alisema Kamati ya PAC na Bunge walifanya kazi nzuri
kwa kurejea ripoti za CAG, Takukuru kuwa fedha hizo ni za umma, hivyo
kilichofanywa na Bunge kwa wahusika ni sahihi.
“Tanesco ni shirika la umma, kama wanadaiwa
inakuwa ni Watanzania ndiyo wanadaiwa, kama wana fedha nyingi ni za
Watanzania, kama hawana fedha ni Watanzania hawana fedha, hivyo hakuna
haja ya kubishana kuwa fedha ni za nani kwa kuwa shirika hilo ni la
umma,” alisema Profesa Moshi.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet),
Cathleen Sekwao alisema, “Bunge limemaliza kazi yake kilichobaki ni
utekelezaji wa maazimio.”
“Bado sijajua kwa nini zile fedha Sh73 bilioni
ambazo wanasema zilipitia Benki ya Stanbic hawakutajwa wahusika nao
wanatakiwa kutajwa ili Watanzania wawajue.”
Aliongeza; “Kila siku tunalalamika hakuna
madawati, vyumba vya madarasa, mishahara ya walimu na maabara sasa fedha
hizo Rais Jakaya Kikwete ahakikishe zinarudi ili zikatatue changamoto
hizi ambazo ni tatizo.”
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق