Kampeni ya kupinga ukatili: Haki itendeke

Katuni
Jumanne wiki hii Ni Tanzania  iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na  maadamano makubwa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na mashirika mbalimbali ya wanaharakati nchini ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili dhidi ya kijinsia hususani kwa watoto na wanawake.
 Mashirika hayo yakiwamo, Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLADF), Mtanadao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Chama cha Wanasheria wa Tanzania (Tawla), Chama cha Wanasheria Zanzibar (Zafela), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mengine yamekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili na ni miongoni mwa walioratibu maandamano hayo.

 Kumekuwapo na mmomonyoko mkubwa wa maadili nchini, jambo ambalo linachangia kasi kubwa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika sehemu zote za Tanzania kwa maana ya Bara na Visiwani.

 Matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekuwa yakiwaathiri wanawake na watoto nchini yahahusu ubakaji, ulawiti, vipigo kwa wanawake, tohara za wanawake na wasichana, ndoa za utotoni na mimba za utotoni. Nyingine ni kuwanyima fursa za elimu watoto wa kike, kuwazuia wanawake kurithi mali, mirathi, talaka, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wanaume kutelekeza familia.

Kampeni hiyo ina umuhimu wake mkubwa katika jamii yetu na kauli mbiu yake ya “Funguka, fichua ukatili wa kijinsia kwa afya ya jamii” ina mantiki na inakwenda na wakati kwa kuwa inalenga kulieleza kwa undani suala la ukatili wa jinsia na athari zake kubwa kwa jamii.

 Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza wakati wa maadamano hayo ni wanawake kuiomba serikali kupigania haki zao kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuwachukulia hatua za kisheria wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia tokana na matukio hayo kukithiri katika jamii.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (Wildaf), Dk. Judith Odunga alisema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku huku kundi linaloathirika zaidi ikiwa ni watoto na wanawake.

Wanaharakati hao wanasema kampeni ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili itaambatana na shughuli mbalimbali zikiwamo za kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia. Vilevile, maonyesho ya programu mbalimbali za asasi zinazolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia na kutoa mada mbalimbali zinazohusiana na ukatili huo.

Kampeni hiyo inaigusa jamii kwa kuwa athari dhidi ya mwanamke ni kitendo hasi kutokana na mwanamke kuwa tegemeo kubwa katika jamii na zaidi katika ngazi ya familia.

Kwa upande wa Tanzania Visiwani, asasi kadhaa zisizo za kiserikali zinazopambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ziliitaka Serikali ya Zanzibar kuchukua hatua dhidi ya wanaochangia na kuendeleza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

 Walisema janga la udhalilishaji wa kijinsia kwa kiasi kikubwa limepelekea waliotendewa ukatili  kupata matatizo ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kukwazwa kimaendeleo.

Wakati wa maadhimisho hayo kila mwaka jamii imekuwa ikiyashuhudia makundi ya wanaharakati yakitumia fursa hiyo pamoja na mambo mengine, kulaani, kutoa elimu ya kupambana na ukatili na kuibua vitendo kadhaa vya ukatili.
Ni jambo la msingi kwa wanaharakati kuibua vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wote wa kampeni hiyo, lakini sisi tunashauri kwamba haki inapaswa kuzingatiwa wakati wa kuwaibua watuhumiwa wa matendo hayo yasiyofaa katika jamii kwa kuhakikisha kuwa nao wanpewa nafasi ya kujitetea badala ya kulaumiwa tu.

Kwa mfano, vyombo vya habari vinavyoripoti matukio hayo viende mbali zaidi kwa kuangalia pande zote za Shilingi; kwa maana ya kuwasikiliza walalamikaji na walalamikiwa kwa kuwa hizo ni tuhuma ambazo hazijatolewa maamuzi na Mahakama. Kwa kufanya hivyo, tunaamini kuwa haki itakuwa imetendeka kwa pande zote.

Hata hivyo, tunazikumbusha serikali zote kusikiliza kilio cha jamii kuhusiana na kasi kubwa ya matukio ya ukatili na kuchukua hatua kwa kuhakikisha kwamba watuhumiwa wanakamatwa, kufikishwa mahakamani na kesi hizo zinaamuliwa kwa muda na kwa haki. Tunasema hivyo kwa kuwa yamekuwapo malalamiko mengi kwamba vyombo vya dola havizipatii kesi hizo kipaumbele.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم