Kashfa ya IPTL, Uchaguzi Mkuu 2015 vyashusha thamani ya Shilingi

Dar es Salaam. Hatua ya wahisani kuzuia Sh1 trilioni za misaada ya kibajeti kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL na wasiwasi wa Uchaguzi Mkuu mwakani, ni miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa kasi thamani ya Shilingi nchini, imefahamika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wasomi na wadau wa biashara nchini walisema sababu nyingine ni uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Januari 2, mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1,586 lakini sasa imepanda hadi Sh1,745. Ikumbukwe kuwa katikati ya mwaka huu, Dola moja ilikuwa ikinunuliwa kwa hadi Sh1,800 katika baadhi ya benki na maduka ya kubadilishia fedha, jambo lililoongeza gharama za ufanyaji biashara na kuongeza bei ya bidhaa.
Escrow
Hivi karibuni, wahisani walitangaza kusimamisha misaada hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na kuchukua hatua.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi alisema hatua iliyochukuliwa na nchi wahisani ya kuzuia fedha za misaada hiyo ambazo zingeingia katika mzunguko wa fedha, imesababisha upungufu wa Dola katika soko la fedha, hivyo kuongezeka thamani.
Alisema iwapo fedha hizo zingekuwa kwenye mzunguko, zingesaidia kupunguza uhaba wa Dola uliopo ambao umesababisha kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kuchangia kupandisha thamani ya Shilingi.
“Hata kitendo cha Tanzania kuuza bidhaa chache nje ya nchi kimechangia mahitaji ya Dola kuongezeka kutokana na uhaba wa fedha hizo hapa nchini,” alisema Dk Ngowi akitaja sababu nyingine ya kuporomoka kwa Shilingi.
Hoja ya Dk Ngowi iliungwa mkono na Meneja wa Fedha wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshindo Ibrahim akisema kuzuiwa kwa fedha hizo za hisani, kumechangia kupaisha thamani ya Dola, licha ya kuwapo tatizo la kuuza bidhaa kidogo nje ya nchi.
“Sisi ni waagizaji wakubwa wa bidhaa kuliko kuuza nje, tunajikuta tunapata Dola kidogo kuliko mahitaji jambo linaloiongeza thamani yake, lakini hili la wahisani kushikilia fedha za bajeti kutokana na sakata la IPTL ni moja ya sababu kubwa kwa sasa,” alisema Ibrahim.
Iwapo wahisani ambao hutoa fedha zao kwa sarafu za kigeni wataziachia, mtaalamu huyo alisema zitasaidia kupunguza wingi wa Shilingi kwa kuwa Dola hizo zinatakiwa kubadilishwa kwa sarafu ya ndani ili zianze kutumika.
Alisema kuna wakati hali hiyo ni kawaida kibiashara.
- Soma zaidi Hapa - Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post