Dar es Salaam. Hatua ya wahisani kuzuia Sh1
trilioni za misaada ya kibajeti kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL
na wasiwasi wa Uchaguzi Mkuu mwakani, ni miongoni mwa sababu za
kuporomoka kwa kasi thamani ya Shilingi nchini, imefahamika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki iliyopita,
wasomi na wadau wa biashara nchini walisema sababu nyingine ni uagizaji
na uuzaji bidhaa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Januari 2, mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa
Sh1,586 lakini sasa imepanda hadi Sh1,745. Ikumbukwe kuwa katikati ya
mwaka huu, Dola moja ilikuwa ikinunuliwa kwa hadi Sh1,800 katika baadhi
ya benki na maduka ya kubadilishia fedha, jambo lililoongeza gharama za
ufanyaji biashara na kuongeza bei ya bidhaa.
Escrow
Hivi karibuni, wahisani walitangaza kusimamisha
misaada hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na
kuchukua hatua.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Prosper Ngowi alisema hatua iliyochukuliwa na nchi wahisani ya kuzuia
fedha za misaada hiyo ambazo zingeingia katika mzunguko wa fedha,
imesababisha upungufu wa Dola katika soko la fedha, hivyo kuongezeka
thamani.
Alisema iwapo fedha hizo zingekuwa kwenye
mzunguko, zingesaidia kupunguza uhaba wa Dola uliopo ambao umesababisha
kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kuchangia kupandisha thamani ya Shilingi.
“Hata kitendo cha Tanzania kuuza bidhaa chache nje
ya nchi kimechangia mahitaji ya Dola kuongezeka kutokana na uhaba wa
fedha hizo hapa nchini,” alisema Dk Ngowi akitaja sababu nyingine ya
kuporomoka kwa Shilingi.
Hoja ya Dk Ngowi iliungwa mkono na Meneja wa Fedha
wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshindo Ibrahim akisema kuzuiwa
kwa fedha hizo za hisani, kumechangia kupaisha thamani ya Dola, licha
ya kuwapo tatizo la kuuza bidhaa kidogo nje ya nchi.
“Sisi ni waagizaji wakubwa wa bidhaa kuliko kuuza
nje, tunajikuta tunapata Dola kidogo kuliko mahitaji jambo linaloiongeza
thamani yake, lakini hili la wahisani kushikilia fedha za bajeti
kutokana na sakata la IPTL ni moja ya sababu kubwa kwa sasa,” alisema
Ibrahim.
Iwapo wahisani ambao hutoa fedha zao kwa sarafu za
kigeni wataziachia, mtaalamu huyo alisema zitasaidia kupunguza wingi wa
Shilingi kwa kuwa Dola hizo zinatakiwa kubadilishwa kwa sarafu ya ndani
ili zianze kutumika.
إرسال تعليق