Baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba wameitaka
serikali ichapishe kwa wingi na kuzisambaza kwa wananchi nakala za
katiba pendekezwa, ili wananchi waisome, waitafakari na kuielewa kabla
ya kuipigia kura ya maoni huku wakitahadharisha uwezekano wa nchi kuwa
na katiba isiyokidhi matarajio na maslahi ya wananchi endapo wataipigia
kura kabla ya kuisoma na kuiielewa.
Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na mfuko wa Mwalimu
Nyerere uliofanyika jijini Dar es Salaam, wajumbe hao akiwemo aliyekuwa
mwenyekiti wa tume hiyo jaji mstaafu Joseph Warioba, wameelezea
kutoridhishwa na tunu za taifa, haki za makundi mbalimbali kama vile
watu wenye ulemavu, wanawake na watoto na baadhi ya vipengele kuondolewa.
Akizungumza katika mdahalo huo, aliyekuwa mjumbe wa tume Bw Hamfrey
Polepole ametaka kuwepo maridhiano ya kikatiba kati ya pande mbili za
muungano ili uwepo muungano unaokubaliwa, unaodumishwa na kulindwa
kikatiba huku akieleza kusikitishwa na kitendo cha kufutwa kwa ibara
muhimu zilizokuwa katika rasimu ya katiba na kushauri ibara hizo
zirejeshwe kwani ndiyo msingi wa katiba inayozingatia maslahi ya
wananchi na taifa imara.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliohudhuria mdahalo huo
na kupata fursa ya kuuliza maswali akiwemo Prof Ibrahimu Lipumba
amesema katiba isiyozingatia maadili na kuweka bayana tunu za taifa
haiwezi kuwa katiba bora itakayodumu kwa miaka mingi ijayo huku baadhi ya
wananchi wakiomba ufafanuzi kwa baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye
rasimu ya pili hasa kile kinachohusu madaraka ya rais.
Hata hivyo mdahalo huo umekuwa na ulinzi mkali wa polisi tofauti na
midahalo mingine ambapo mwandishi alishuhudia wahudhuriaji wakiwa
wanakaguliwa na vifaa maalum kabla ya kuingia ndani.
إرسال تعليق