Tumeshuhudia kwa mara ya kwanza tangu nchi yetu ipate uhuru
mwaka 1961, mihimili ya dola, yaani Mahakama, Bunge na Serikali
ikigongana na kukinzana katika suala muhimu la kitaifa, huku ikiibua
mashaka kuhusu tafsiri ya dhana ya mgawanyo wa madaraka miongoni mwa
mihimili hiyo. Hali hiyo imetokana na amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam iliyodaiwa kuzuia Bunge kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu kashfa ya uchotwaji wa Sh306
bilioni kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati mahakama hiyo ikidaiwa kutoa amri hiyo
ambayo ingedumu hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa katika mahakama hiyo
na kampuni ya kufua umeme ya IPTL na kampuni tanzu ya Pan African Power
Solutions (PAP) itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi, Bunge lilisema
ripoti hiyo lazima ijadiliwe kwa kuwa linayo mamlaka kikatiba kuendesha
shughuli zake bila kuingiliwa na mamlaka nyingine yoyote, ikiwamo
Mahakama. Bunge lilisimamia kwenye ibara ya 100 (1) katika Katiba
inayosema kuwa, kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu
katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote
katika Jamhuri ya Muungano au katika Mahakama au mahali pengine nje ya
Bunge.
Lakini ukweli uliojitokeza baadaye ni kwamba
Mahakama Kuu haikuzuia Bunge kujadili ripoti hiyo ya CAG kuhusu kashfa
ya akaunti ya Escrow. Ukweli ni kwamba mkanganyiko uliojitokeza
ulitokana na Bunge kutoa matamko kuhusu kuwapo amri ya mahakama
iliyodaiwa kuzuia mjadala wa ripoti ya CAG bila kuwa na nakala halisi ya
hukumu husika. Hivyo, matamko ya wabunge yalikuwa hisia tu zisizokuwa
na ukweli wowote. Ndiyo maana awali tulihoji kama kweli kuna mahakama
yoyote nchini inayoweza kutoa amri inayokwenda kinyume na ibara hiyo ya
100 (1)ya Katiba inayotoa kinga kwa Bunge ili lisiingiliwe kwa njia
yoyote katika kuendesha shughuli zake.
Ni kwa mantiki hiyo tunasema huenda amri ya
Mahakama Kuu ilitafsiriwa vibaya kutokana na kujadiliwa bungeni na bila
kwanza kuona nakala halisi ya hukumu ya mahakama hiyo. Inawezekana
kabisa kwamba huenda hali hiyo ilisababishwa na mihemko ya kisiasa
iliyotokana na unyeti wa kashfa hiyo ya akaunti ya Escrow. Ukweli ni
kuwa, pamoja na juhudi za IPTL na PAP kuomba mahakama kuzuia mjadala huo
bungeni, hukumu iliyotolewa na majaji hao ilisema kila kitu kiendelee
kama kilivyopangwa, hivyo hakuna mahali popote katika amri hiyo, ambapo
Bunge lilikatazwa kuijadili ripoti hiyo ya CAG.
Ingekuwa kweli kwamba mahakama ililizuia Bunge
kujadili ripoti ya CAG, hapana shaka kwamba Mahakama ingekuwa imevunja
Katiba kwa kuliingilia Bunge lisifanye shughuli zake. Pia lawama
zingeelekezwa kwa mhimili huyo kwa kusababisha mkanganyiko huo, kama
ambavyo zimekuwapo lawama kwa baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufani kuandika hukumu kisiasa, kwa maana ya
kuzungukazunguka na kutoa hukumu ambazo siyo tu hazieleweki, bali pia
zenye maudhui yanayochanganya.
Ni katika muktadha huo tunasema kuna umuhimu wa
kuanzisha Mahakama ya Katiba hapa nchini, ambayo jukumu lake litakuwa
kushughulikia kesi na mashauri ya kikatiba iwapo yatatokea. Ripoti
kuhusu kashfa ya Escrow iliyowasilishwa bungeni jana ni somo tosha kwa
kila mmoja wetu na mihimili yote ya dola.
Post a Comment