Mtanzania unafanya nini sakata la Tegeta Escrow?

Kwa mara nyingine tena, Serikali ya Tanzania imeingia doa mbele ya wananchi wake pamoja na wahisani wa maendeleo.
Wizi wa Dola 250 milioni za Marekani sawa na kiasi cha zaidi ya bilioni 350 za Tanzania zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, Tegeta Escrow una mgusa kila mpenda maendeleo ambaye kwa namna moja ama nyingine fedha yake inatumika kuiwezesha Serikali katika shughuli zake za kila siku.
Wizi huu unaikuta nchi ikiwa katika wimbi la matatizo ikiwamo kushindwa kwa Serikali kugharimia sekta ya afya na kusababisha wagonjwa kukosa huduma za msingi kama vile ukosefu wa dawa kwa ajili ya matibabu. Ni katika kipindi ambacho wanafunzi wengi wa elimu ya juu wamekosa mikopo kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali.
Huku maisha ya Watanzania wa kawaida yanazidi kuwa magumu zaidi, hali ni tofauti kabisa kwa viongozi wa taifa pamoja na familia zao ambao wao wanaishi kama vile wako ughaibuni wakiwa hawana tone la shida.
Imekuwa ikidhaniwa kama vile ni hoja ya wanasiasa fulani haswa David Kafulila (Mbunge wa Kigoma Kusini) ambaye aliamua kulibeba suala hili tangu mwanzo mpaka leo.
Sikatai kwamba huko kwenye siasa ndiko hoja ilipoibukia na pengine Bunge ndio chombo sahihi kimamlaka katika kudai uwajibikaji kwa wahusika wa Tegeta Escrow lakini sidhani kama ni sahihi kuliacha suala hili kwa wanasiasa peke yake hapa ililipofikia.
Asasi za kirai, vyombo vya habari na makundi mbalimbali yenye nguvu katika jamii, ni muda mwafaka sasa kuongeza nguvu ili sauti dhidi ya ufisadi wa escrow zisikike zaidi bila kujali kusingiziwa kubeba hoja ya kisiasa kwani suala hili siyo la kisiasa tena.
Kuna haja ya kushinikiza nyaraka zote ziwekwe wazi, ushahidi upatikane, watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki.
Asasi zinazosimamia haki za makundi mbalimbali kama vile wanawake na watoto, wazee, haki za kiraia, haki za wafanyakazi na kadhalika nina aamini kuwa makundi yote hayo yameumizwa na ufisadi wa escrow aidha moja kwa moja ama kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.
Nakumbuka maandamano ya wanaharakati wakati wa mgomo wa madaktari, msukumo mkubwa ulikuwa ni kuokoa maisha ya watu sasa kwa nini leo hii waachiwe wanasiasa wakilumbana ili hali hospitali hazina madawa kutokana ufisadi huu wa escrow, watu wanangapi wanakufa kwa kukoswa madawa?
Nchi yetu tunaijua wenyewe, mara nyingi masuala yanaoibuliwa na wapinzani hujengewa mazingira ya kuonekana yana maslahi ya kisiasa tu na hayana ukweli ndani yake. Kurushiana mpira baiana ya mamlaka moja na nyingine ni michezo ya kawaida ambayo huwa inafanywa ili muda upite watu wasahau jambo.
Wanafahamu kuwa chaguzi za serikali za mitaa zinakuja na hata baada ya hapo kuna vuruga za hapa na pale za kuelekea kura ya maoni ya katiba pamoja na uchaguzi mkuu hapo mwakani na sote tunajua kuwa wanasiasa punde watakuwa bize na chaguzi hivyo huu ndio muda maalumu kwa kila kitu kushughulikiwa kikamilifu.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post