Wizi wa Dola 250 milioni za Marekani sawa na kiasi
cha zaidi ya bilioni 350 za Tanzania zilizokuwa katika akaunti maalumu
ya IPTL, Tegeta Escrow una mgusa kila mpenda maendeleo ambaye kwa namna
moja ama nyingine fedha yake inatumika kuiwezesha Serikali katika
shughuli zake za kila siku.
Wizi huu unaikuta nchi ikiwa katika wimbi la
matatizo ikiwamo kushindwa kwa Serikali kugharimia sekta ya afya na
kusababisha wagonjwa kukosa huduma za msingi kama vile ukosefu wa dawa
kwa ajili ya matibabu. Ni katika kipindi ambacho wanafunzi wengi wa
elimu ya juu wamekosa mikopo kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali.
Huku maisha ya Watanzania wa kawaida yanazidi kuwa
magumu zaidi, hali ni tofauti kabisa kwa viongozi wa taifa pamoja na
familia zao ambao wao wanaishi kama vile wako ughaibuni wakiwa hawana
tone la shida.
Imekuwa ikidhaniwa kama vile ni hoja ya wanasiasa
fulani haswa David Kafulila (Mbunge wa Kigoma Kusini) ambaye aliamua
kulibeba suala hili tangu mwanzo mpaka leo.
Sikatai kwamba huko kwenye siasa ndiko hoja
ilipoibukia na pengine Bunge ndio chombo sahihi kimamlaka katika kudai
uwajibikaji kwa wahusika wa Tegeta Escrow lakini sidhani kama ni sahihi
kuliacha suala hili kwa wanasiasa peke yake hapa ililipofikia.
Asasi za kirai, vyombo vya habari na makundi
mbalimbali yenye nguvu katika jamii, ni muda mwafaka sasa kuongeza nguvu
ili sauti dhidi ya ufisadi wa escrow zisikike zaidi bila kujali
kusingiziwa kubeba hoja ya kisiasa kwani suala hili siyo la kisiasa
tena.
Kuna haja ya kushinikiza nyaraka zote ziwekwe wazi, ushahidi upatikane, watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki.
Asasi zinazosimamia haki za makundi mbalimbali
kama vile wanawake na watoto, wazee, haki za kiraia, haki za wafanyakazi
na kadhalika nina aamini kuwa makundi yote hayo yameumizwa na ufisadi
wa escrow aidha moja kwa moja ama kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.
Nakumbuka maandamano ya wanaharakati wakati wa
mgomo wa madaktari, msukumo mkubwa ulikuwa ni kuokoa maisha ya watu sasa
kwa nini leo hii waachiwe wanasiasa wakilumbana ili hali hospitali
hazina madawa kutokana ufisadi huu wa escrow, watu wanangapi wanakufa
kwa kukoswa madawa?
Nchi yetu tunaijua wenyewe, mara nyingi masuala
yanaoibuliwa na wapinzani hujengewa mazingira ya kuonekana yana maslahi
ya kisiasa tu na hayana ukweli ndani yake. Kurushiana mpira baiana ya
mamlaka moja na nyingine ni michezo ya kawaida ambayo huwa inafanywa ili
muda upite watu wasahau jambo.
Wanafahamu kuwa chaguzi za serikali za mitaa
zinakuja na hata baada ya hapo kuna vuruga za hapa na pale za kuelekea
kura ya maoni ya katiba pamoja na uchaguzi mkuu hapo mwakani na sote
tunajua kuwa wanasiasa punde watakuwa bize na chaguzi hivyo huu ndio
muda maalumu kwa kila kitu kushughulikiwa kikamilifu.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق