Kikosi bora Ligi Kuu Bara msimu huu


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), imesimama kwa wiki saba kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Swaziland dhidi ya Taifa Stars, usajili wa dirisha dogo, mashindano ya Kombe la Uhai yanayoshirikisha Timu B za timu za Ligi Kuu na michuano ya Chalenji ambayo hata hivyo inaonekana kukwama kutokana na kukosa nchi mwenyeji baada ya Ethiopia kujitoa.
Ligi imesimama zikiwa zimechezwa mechi 49 za raundi ya kwanza hadi ya saba, mabao 91 yakifungwa (wastani wa mabao 1.86 kwa mechi), 50 yakifungwa na timu mwenyeji (uwanja wa nyumbani) na 41 yakifungwa na timu ngeni, ikiwa ni mabao machache ikilinganishawa na msimu uliopita wa VPL kwani hadi hatua hiyo tayari mabao 101 yalikuwa yametiwa kambani (wastani wa mabao mawili kwa mechi).

Baadhi ya timu na wachezaji wamekuwa na msimu mbaya huku nyota wa Mtibwa Sugar na timu hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili mfululizo 1999 na katika mwaka wa mabadiliko ya karne, waking'ara kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 15, mbili nyuma ya Azam FC waliopo nafasi ya pili na Yanga wanaokamata nafasi ya tatu.

Makala haya yanaangalia ubora wa wachezaji hadi raundi ya saba ya VPL msimu huu kulingana na nafasi wanazocheza kwa mujibu wa NIPASHE.

1. Said Mohamed (Mtibwa)
Amefanya kazi nzuri msimu huu, Mtibwa ikifungwa mabao matatu katika mechi zote saba walizocheza hadi sasa wakizifunga Yanga 2-0, Ndanda FC 3-1, Mgambo Shooting 1-0, Mbeya City 2-0, wakatoka sare mbili za bao moja dhidi ya Simba na Kagera Sugar na kutoka suluhu dhidi ya 'wababe wao wa kihistoria', Polisi Morogoro.

2. Salum Kimenya (Prisons)
Timu nyingi duniani kwa sasa zinawatumia mabeki wa pembeni kushambulia wakisaidiana na mawinga. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekuwa mpishi mzuri wa mabeki wa pembeni katika miaka yake 18 kwenye klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England.

Katika mechi zilizopita za VPL, Kimenya amefanya kazi nzuri katika kikosi cha David Mwamwaja kama beki wa pembeni akipandisha mashambulizi ya timu akishirikiana na mawinga wa Tanzania Prisons, hususan Hamis Maingo. Kimenya alithibitisha ubora wake hasa katika mechi dhidi ya JKT Ruvu na Simba kwenye Uwanja wa Sokoine na pengine, ni kwa sababu hii Simba wameamua kusaka saini yake kipindi hiki cha dirisha dogo.

3. Shomari Kapombe (Azam FC), akiwa Simba alikuwa akitumika kama beki wa kati lakini aliyekuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen alipendelea kumtumia kama beki wa pembeni na alifanya kazi nzuri. Alipika bao kali katika mechi iliyopita ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa. Baada ya kufanikiwa kumsajili, Azam FC wamekuwa wakimtumia katika nafasi hiyo ya beki wa pembeni na amefanya kazi nzuri katika kulilinda lango la kikosi cha Mcameroon Joseph Omog na kupandisha mashambulizi msimu huu.

4. Aggrey Morris (Azam FC)
Mchango wake si katika vikosi vya Taifa Stars na Zanzibar Heroes pekee, bali amekuwa chachu kwa mafanikio ya Azam FC. Msimu huu amefanya vizuri zaidi akifanya kazi ya washambuliaji kwa kufunga mabao mawili hadi sasa.

5. Salim Mbonde
Ukuta wa Mtibwa Sugar umeimarika kutokana na uwezo mkubwa alionao mchezaji huyu akisaidiana na beki mwenzake wa kati Andrew Vincent na wa pembeni David Luhende na Hassan Ramadhan. 

6. Jonas Mkude (Simba)
Simba imekuwa na matokeo mabovu tangu miezi nane iliyopita ilipoifunga 3-2 Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa lakini ubora wa kiungo huyu umeendelea kuonekana. Mkude anajua kukaba kwa nidhamu, ana nguvu na ni mzuri wa kupiga mashuti.

7. Hamis Maingo (Prisons)
Uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga na kukimbia kwa kasi, ni miongoni mwa sifa nyingi alizonazo winga huyo wa Tanzania Prisons. Amekuwa moyo wa timu hiyo ya magereza. Alifanya vizuri zaidi katika mechi waliyolala 2-1 nyumbani dhidi ya JKT Ruvu lakini ubora wake akaudhihirisha katika mechi aliyofunga bao la kusawazisha dhidi ya Simba akitokea benchi.

8. Shaban Nditi (Mtibwa)
Unapowazungumzia viungo matata msimu huu, bila shaka hutasita kumtaja kiungo huyu. Amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Mtibwa akicheza kwa miaka 13 Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Msimu huu Nditi amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya wakatamiwa hao wa Manungu, Turiani.

9. Emmanuel Okwi (Simba)
Mganda huyu ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kumiliki mpira. Amefanya kazi nzuri katika kikosi cha Simba msimu huu akifunga mabao matatu akifuatwa na Shaban Kisiga aliyefunga mabao mawili.

10. Ame Ally Amour (Mtibwa)
Anaongoza safu ya wafumania nyavu akiwa na mabao manne sawa na Didier Kavumbagu wa Azam FC, Rama Salim wa Coastal Union na Danny Mrwanda wa Polisi Morogoro. Ame anayehusishwa kwenda Simba na Yanga kipindi hiki cha dirisha dogo, ana miguu inayojua lango lilipo.

11. Kipre Tchetche (Azam FC)
Pacha huyo wa kiungo Michael Bolou (wa Azam FC pia) amekuwa akicheza kama straika na kiungo mshambuliaji kiasi cha 'kuupofusha' uongozi wa Azam na kufanya uamini kwamba timu yao iko vizuri katika safu ya kiungo ilhali haina kiungo mshambuliaji mzuri. Tchetche amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Azam ndiyo maana anapokosekana kunakuwa shubiri. Azam FC imepoteza mechi mbili mfululizo msimu huu dhidi ya JKT Ruvu na Ndanda FC ambazo Tchetche hakucheza kwa sababu hakuwapo nchini.

WACHEZAJI WA AKIBA
1. Deogratius Munishi Dida (Yanga)
2. Hassan Ramadhan (Mtibwa)
3. Nadir Haroub 'Cannavaro' (Yanga)
4. Salum Abubakar 'Sure Boy' (Azam)
5. Simon Msuva (Yanga)
6. Rama Salim (Coastal)
7. Malimi Busungu (Mgambo)

Kocha: Mecky Mexime
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم