Kila kona wataka ‘watuhumiwa’ escrow wafilisiwe

 
Dar/Z’bar/mikoani. Siku moja baada ya Kamati ya PAC kuweka hadharani uchunguzi wa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, watu wa kada mbalimbali wamependekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Zanzibar
Viongozi wa upinzani Zanzibar wamesema wote waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ufisadi kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow wafukuzwe pamoja na kufunguliwa mashtaka badala ya kuendelea kusubiri msimamo wa Rais katika jambo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Viongozi wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na Tadea walisema kiwango cha fedha kilichoibiwa ni kikubwa na haikubaliki kwa nchi inayoheshimu misingi ya utawala bora.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Zanzibar, Ambar Khamis Haji alisema viongozi walioguswa na ripoti ya uchunguzi lazima wawe watu waugwana waondoke katika nyadhifa zao wenyewe wasubiri sheria ichukuliwe mkondo wake.
Alisema pamoja na viongozi wa dini na majaji walioguswa katika kashfa ni wakati mwafaka na wao kujiuzulu kutokana na kitendo chao cha kudhalilisha mamlaka wanazoziongoza wakati wao wanatakiwa kuwa mfano bora katika jamii. “Pamoja na kwamba fedha za sadaka huwa hazichagui fedha halali au chafu hatuamini kama zilikuwa za kanisa kutokana na kutumika kwa akaunti ya mtu binafsi,” alisema Ambar.
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdallah alisema Serikali nzima inapaswa kujiuzulu kutokana na ukubwa wa kashfa.
“Rais wetu ni mtendaji siyo kama mfalme, haiwezekani kufanyike wizi mkubwa kama huo bila ya kufahamu na kuchukua hatua mapema, Serikali nzima ivunjwe kuitishwe uchaguzi,” alisema Bimani.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Issa Mohamed alisema wakati umefika kwa wananchi kujifundisha na kuwa makini wanapofanya uamuzi ya viongozi kwa sababu CCM imeshindwa kupambana na vitendo vya ufisadi katika Serikali yake.
Alisema inasikitisha, wakati Sh306 bilioni zikipotea, wananchi wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kuanguka huduma za jamii.
“Dawa hakuna wanafunzi wanasoma chini ya sakafu huku wengine wakikosa mikopo ya elimu ya juu, wazazi wakilazwa chini kutokana na uhaba wa vitanda hospitali za Serikali.
“Katika misingi ya utawala bora wanahitajika kujiuzulu kabla ya kufukuzwa na Rais ili sheria ichukue mkondo wake na mali zao zitaifishwe,” alisema Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم