Kondomu feki za mamilioni zateketezwa

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jana liliteketeza kondomu feki aina ya Mood vipande 601,100 vyenye thamani ya Sh. milioni 29.7 ambazo zimebainika kutengenezwa India.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya zoezi hilo lililofanyika katika eneo la Pugu Dampo, Ofisa Ubora kutoka TBS, Athuman Kisumo, alisema kondomu hizo ziliteketezwa baada ya kuwasili nchini na kubainika hazina ubora na hazifai kwa matumizi.

Vipimo vya maabara vimethibitisha bidhaa hiyo imekosa ujazo wa hewa pamoja na matundu ya maji, alisema.

“Tutaendelea na ukaguzi wetu kila mara ili tuweze kubaini bidhaa hafifu, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mlaji analindwa na anakuwa salama wakati wote,” alisema.

Kwa mujibu wa ofisa huyu, kondomu hizo ziliagizwa iliagizwa na kiwanda cha Planet Phamaceutical kwa ajili ya kuzisambaza kwenye maduka na jumla na rejareja ndipo ilipobainika hazina viwango vinavyopendekezwa na TBS.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa vipimo vya maabara, bidhaa hiyo inapasuka haraka na haiwezi kuhimili mikiki, hivyo ni rahisi mtu kupata ujauzito asio tegemea au kupata maambukizi ya Ukwimu na magonjwa ya zinaa.

Afisa Uhusiano wa Kiwanda cha Planet Phamaceutical, Richard Muyombo, alisema bidhaa hiyo waliagiza Agosti mwaka jana na kwamba wanajihusisha na uuzaji wa dawa na vifaa tiba.

Alisema TBS inatakiwa kuhakikisha inakuwa na mawakala wao ili kuzuia mizigo isiingie nchini na siyo kusubiri hadi ifikishwe nchini na kuteketezwa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم