Kuondoka kwa Massawe ni tiba ya mgogoro wa Kagasheki na Dk Amani?

Kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera, hususan mjini Bukoba itawachukua muda mrefukusahau jina la mkuu wa mkoa aliyeondoka,  Kanali Fabian Massawe wanapokuwa kwenye mijadala ya kila siku.
Wengi wanaamini kuondoka kwake ni zaidi ya tukio la kawaida lenye uhusiano wa moja kwa moja na uhasama wa kisiasa kati ya mbunge wa Jimbo la Bukoba, Balozi Hamis Kagasheki na Meya Dk Anatory Amani.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili umesababisha hata viongozi wa kitaifa kupata kigugumizi kufanya mikutano ya hadhara mjini Bukoba kwa kutokuwa na majibu ya kuridhisha makundi yenye uhasama.
Kiongozi pekee aliyepata ujasiri wa kusimama na kuhutubia jukwaani kwenye Uwanja wa Mayunga ni naibu katibu mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba aliyeanza  kwa kujisalimisha kuwa haungi mkono upande wowote.
Shauku ya wananchi ilikuwa ni  kufahamu viongozi wa kitaifa wanaunga mkono kiongozi yupi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani. Hata hotuba zao zisingekuwa na maana kama wasingetoa msimamo kuhusu sakata baina ya makundi hayo.
Inaonekana kilichofanyika ni kama sehemu ya mpango mkakati wa kutuliza hali ya kisiasa katika Jimbo la Bukoba, hasa baada ya mbunge huyo  kumtuhumu  Kanali Massawe kuwa anamuunga mkono hasimu wake.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa aliunga mkono utekelezaji wa mradi  wa soko, upimaji wa viwanja na ujenzi wa kituo kipya cha mabasi ambayo kimsingi ndiyo malalamiko ya Balozi Kagasheki.
Katika kipindi cha mgogoro, Balozi Kagasheki hakuhudhuria sherehe za kitaifa zilizoratibiwa na mkuu wa mkoa na hata alipokosekana kwenye sherehe za siku ya Mwalimu kitaifa zilizofunguliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mjini Bukoba, haikutolewa sababu.
Hata katika tukio la hivi karibuni lililoongozwa na Naibu Waziri (Tamisemi) Kassimu Majaliwa la harambee ya kuchangia ujenzi wa maabara katika Manispaa ya Bukoba, hakuna sababu iliyotolewa ya kutohudhuria kwake.
Aliyekuwa mkurugenzi wa manispaa, Adoh Mapunda alisema mbunge ametoa Sh30 milioni, ingawa kama ilivyothibitishwa na mkurugenzi fedha hizo zilitoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zilizotumwa tangu Septemba.
Kwa upande mwingine mabadiliko yanahusishwa na masilahi ya siasa za Kanda ya Ziwa ndani ya CCM. Kwa kuwa John Mongela anatoka Mkoa wa Mwanza inawezekana amesogezwa karibu  na majimbo ya Nyamagana na Ilemela yanayoongozwa na Chadema.
Siku ya kukabidhiwa ofisi alisema hakuja na miujiza zaidi ya kumtaka kila kiongozi kuwajibika kwa nafasi yake. Kwamba  anataka siasa za  maendeleo na siyo mgeni katika fani hiyo kwani amezaliwa katika siasa.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post