Kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera, hususan mjini Bukoba itawachukua
muda mrefukusahau jina la mkuu wa mkoa aliyeondoka, Kanali Fabian
Massawe wanapokuwa kwenye mijadala ya kila siku.
Wengi wanaamini kuondoka kwake ni zaidi ya tukio
la kawaida lenye uhusiano wa moja kwa moja na uhasama wa kisiasa kati ya
mbunge wa Jimbo la Bukoba, Balozi Hamis Kagasheki na Meya Dk Anatory
Amani.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili
umesababisha hata viongozi wa kitaifa kupata kigugumizi kufanya mikutano
ya hadhara mjini Bukoba kwa kutokuwa na majibu ya kuridhisha makundi
yenye uhasama.
Kiongozi pekee aliyepata ujasiri wa kusimama na
kuhutubia jukwaani kwenye Uwanja wa Mayunga ni naibu katibu mkuu wa CCM
Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba aliyeanza kwa kujisalimisha kuwa haungi
mkono upande wowote.
Shauku ya wananchi ilikuwa ni kufahamu viongozi
wa kitaifa wanaunga mkono kiongozi yupi kati ya Balozi Kagasheki na Dk
Amani. Hata hotuba zao zisingekuwa na maana kama wasingetoa msimamo
kuhusu sakata baina ya makundi hayo.
Inaonekana kilichofanyika ni kama sehemu ya mpango
mkakati wa kutuliza hali ya kisiasa katika Jimbo la Bukoba, hasa baada
ya mbunge huyo kumtuhumu Kanali Massawe kuwa anamuunga mkono hasimu
wake.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa aliunga mkono utekelezaji
wa mradi wa soko, upimaji wa viwanja na ujenzi wa kituo kipya cha
mabasi ambayo kimsingi ndiyo malalamiko ya Balozi Kagasheki.
Katika kipindi cha mgogoro, Balozi Kagasheki
hakuhudhuria sherehe za kitaifa zilizoratibiwa na mkuu wa mkoa na hata
alipokosekana kwenye sherehe za siku ya Mwalimu kitaifa zilizofunguliwa
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mjini Bukoba, haikutolewa sababu.
Hata katika tukio la hivi karibuni lililoongozwa
na Naibu Waziri (Tamisemi) Kassimu Majaliwa la harambee ya kuchangia
ujenzi wa maabara katika Manispaa ya Bukoba, hakuna sababu iliyotolewa
ya kutohudhuria kwake.
Aliyekuwa mkurugenzi wa manispaa, Adoh Mapunda
alisema mbunge ametoa Sh30 milioni, ingawa kama ilivyothibitishwa na
mkurugenzi fedha hizo zilitoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo
zilizotumwa tangu Septemba.
Kwa upande mwingine mabadiliko yanahusishwa na
masilahi ya siasa za Kanda ya Ziwa ndani ya CCM. Kwa kuwa John Mongela
anatoka Mkoa wa Mwanza inawezekana amesogezwa karibu na majimbo ya
Nyamagana na Ilemela yanayoongozwa na Chadema.
Siku ya kukabidhiwa ofisi alisema hakuja na
miujiza zaidi ya kumtaka kila kiongozi kuwajibika kwa nafasi yake.
Kwamba anataka siasa za maendeleo na siyo mgeni katika fani hiyo kwani
amezaliwa katika siasa.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق