Dar es Salaam. Baada ya tetesi kuwa ameachana
na mumewe, mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee amesema leo
anajitokeza kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki wake kwani wakati wa
kufanya hivyo umewadia.
Mwimbaji huyo wa wimbo “Yahaya” anayemiliki tuzo
30 za muziki, amejigamba kuwa hivi sasa yupo bize na kazi, kwani
anatarajia kuachia wimbo matata alioupa jina la “Forever” ambao
utaambatana na uzinduzi wa video yake Novemba 28.
“Sina habari na mtu na nitaendelea kuwa komando,
kilichopo watu wasubiri kuona nitawapa nini maana leo ndiyo naachia
wimbo huu, nina mengi ya kuzungumza nao pale nitakapotambulisha kibao
hicho, watege tu masikio yao,” alisema Lady Jaydee.
Alisema anataraji kwamba wimbo huo mpya utapendwa
na mashabiki wake ikiwa ni moja ya mikakati yake kabambe ya kuwafikia
washabiki kwa ukaribu zaidi.
“Watarajie burudani waliyoizoea, nitaachia wimbo
wangu leo Jumatatu na video yake nitaizindua Ijumaa na mashabiki
watakaohudhuria utambulisho huu watapata bahati ya kuiona video ya
“Forever” kwa mara ya kwanza,” alisema Jaydee.
Jaydee aliyepata kutamba na vibao kadhaa kwa
kipindi cha takriban miaka 14, amesema wimbo huo amemshirikisha
mwanamuziki wa regge, Dabo ambaye pia ni mdogo wake.
“Ni wimbo wa mapenzi ambao utabamba, kazi hii imetengenezwa na prodyuza yuleyule Man Water wa Combination Sounds,” alisema.
Alisema pamoja na muziki, ataendelea kuisadia
jamii kama ambavyo amekuwa akifanya kila siku na mazingira yakiendelea
kuruhusu. “Mahitaji ya jamii ni mengi ila kila kinachowezekana basi Lady
Jaydee atafanya kama msaada wa madawati nilioutoa Shinyanga.”
Hata hivyo, nyota huyo hakutaka kuzizungumzia tetesi zilizoenea kuwa ameachana na mumewe.
Lady Jaydee amewahi kutamba na vibao kadhaa huku
akiwa na albamu tano ikiwamo, Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005),
Shukrani (2007) na The Best of Lady Jaydee (2012).
إرسال تعليق