MNADHIMU wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu, amemvaa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG), Jaji Fedrick Werema kuwa ameliingiza hasara taifa kwa kushindwa kuzuia wizi wa fedha zaidi y ash bilioni 300, zilizohifadhiwa katika Akaunti ya Escrow, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) .
Amesema ameshindwa kuchukua hatua zozote dhidi ya mawaziri wa sasa na wa zamani wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na majaji wa Mahakama Kuu ambao wametajwa kuwa miongoni mwa watu waliovuna mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Escrow.
Lissu alisema hayo juzi bungeni wakati alipokuwa akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2014.
Lissu alisema kama Bunge lingepitisha kifungu cha II hadi cha XXVIII ambacho kilikuwa kinampa nguvu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuingilia kesi yoyote ya taasisi au mashirika ya umma mahakamani ilikuwa ni sawa na kiini macho.
Alisema pamoja na kuwepo kwa kifungu hicho ndani ya Katiba ya nchi lakini bado imekuwa sawa na kiini macho hasa kwa kitendo cha kuwepo kwa nyaraka zinazothibitisha ufisadi serikalini au matumizi mbaya ya madaraka kama ilivyotokea wakati wa kashfa ya Richmond/Dowans au Akaunto ya EPA pamoja na ufisadi wa sasa wa Akauti ya Escrow ya IPTL ambazo zingetolewa mahakamani.
“Mheshimiwa Mwenyekiti haya ni majigambo ya bure kwani, katika matukio mengi na makubwa ambayo yameliingizia Taifa hili hasara ya mabilioni ya fedha na kulichafua Taifa letu mbele ya jumuiya za kimataifa, Mwanasheria Mkuu amekuwa mhusika muhimu kama sio mkuu katika kashfa ya Escrow.
Akitolea mfano alisema katika kashfa inayoendelea sasa ya Akaunti ya Escrow, Mwanasheria Mkuu Mkuu, ameshindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya mawaziri wa sasa na wa zamani wa Serikali ya CCM, Mwanasheria Mkuu wa zamani, majaji wa Mahakama Kuu ambao wametajwa kuwa miongoni mwa waliovuna mabilioni ya fedha za Akaunti hiyo.
Aidha alisema mtangulizi wake katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pia alishindwa kuchukua hatua yoyote kwa mawaziri na watendaji wa ngazi za juu ‘waliovuna’ mabilioni ya Richmond/Dowans mwaka 2007/08.
Lissu alisema kabla ya hapo Mwansheria Mkuu huyo alishindwa kuchukua hatua dhidi ya Mwanasheria Mkuu mwenzake aliyemtangulia (Chenge), ‘aliyekatiwa’ mgawo wa ‘vijisenti vya rada’ wakati Mwanasheria Mkuu mwenzake wa Uingereza kupitia Serious Fraud Office(SFO), ya nchi hiyo ikiwashughulikia mafisadi wa kiingereza walihusika na kashfa hiyo.
“Kashfa hiyo iliyoliingizia Taifa letu hasara ya mabilioni ya fedha za umma na kutupaka matope ya ufisadi duniani kote. Yote haya ni nje kabisa mikataba mingi ya kifisadi katika sekta mbalimbali za uchumi wa nchi yetu ambayo Serikali imeingia kwa sababu ya ushauri hafifu na usiofaa wa Mwanasheria Mkuu.
“Kama ilivyokuwa imeombwa na Serikali hii ya CCM kungepanua uwanja zaidi kwa Mwanasheria Mkuu kuendeleza hujuma dhidi ya masilahi halisi ya nchi yetu kwa kuyaingiza mashirika na taasisi nyingine za umma katika makucha ya Sheria ya Mashauri ya Serikali,” alisema Lissu.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema Mwanasheria Mkuu alihoji uhalali wa Shirika Hodhi la Serikali (CHC), kuwalipa mawakili wake wa kujitegemea Sh milioni 855 kama malipo ya mawakili katika kesi 338 za shirika hilo zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni 373.264 kwa maneno ya Mwanasheria Mkuu mwenyewe.
“Kama taasisi na mashirika hayo yana mawakili wenye uzoefu iweje waajiri mawakili hao wa kijitegemea na kutumia kiasi kama hicho cha fedha. Malipo yaliyolalamikiwa na Mwanasheria Mku ni sawa na asilimia 0.22 ya thamani ya kesi zote.
“Kauli hii pekee inaonyesha kwamba Mwanasheria Mkuu ameteleza vibaya kisheria. Ili isonekane kwamba tunamdhalilisha Mwanasheria Mkuu bila sababu yoyote ya msingi tunaomba kufafanua kauli hii.
“…Utaratibu wa malipo kwa mawakili umewekwa na kanuni za malipo ya mawakili na maamuzi ya gharama za mashauri za miaka ya 1991. Kwa waliogombaniwa ambalo thamani yake ni Shilingi milioni tatu au zaidi, ni asilimia tatu ya thamani ya shauri husika,” alisema
Alisema kutokana na hali hiyo kama mawakili wa keso zote zenye thamani iliyotajwa na Mwanasheria Mkuu, basi malipo yao halali yangekuwa takriban Sh bilioni 11.198 balada ya kulipa mabilioni halali.
Jaji Werema
Awali akiwasilisha Muswada wa mabadiliko hayo ya Sheria mbalimbali bungeni, ambao umelenga kufanya marekebisho katika sheria 32 kwa lengo la kuimarisha matumizi ya sheria hizo ili kuongeza masharti mapya katika sheria.
“Muswada huu ulikuwa umegawanyika katika sehemu kuu Thelathin na tatu, baada ya marekebisho yakiyofanywa sasa Muswada utakuwa na sehemu tano. Baada ya majadiliano ya kamati ya Katiba, Sheria na Utawala Serikali imeridhia.
“Sehemu ya pili ya Muswada ilikuwa ni 29 kabla ya marekebisho yaliyofanywa na inapendekeza marekebisho katika sheria ya mbolea, sura ya 378 na ibara ya 58 ya muswada,” alisema Jaji Werema
Alisema sehemu tano ya muswada ilikuwa ni sehemu ya 33 ya marekebisho na inapendekeza kwenye sheria ya huduma za maji na usafi na mazingira sura ya 272 kwa mujibu wa marekebisho katika sehemu ya kifungu cha 59.
- Tanzania Daima
Post a Comment