Mawaziri watoswa

Mawaziri watoswa
  • CCM yabariki waondoke kunusuru chama
  • Wamo Werema, Tibaijuka, Maswi, Muhongo
  • IPTL yaathiri harakati za Mizengo Pinda 2015





KAMATI ya uongozi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imependekeza viongozi waliotajwa kuhusika katika kashfa  ya kuchota fedha zaidi ya sh bilioni 321 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, wajiuzulu.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kamati hiyo iliyokutana juzi usiku, ilipendekeza watuhumiwa hao wajiuzulu ili kukinusuru chama pamoja na serikali inayopakwa matope kwa makosa ya watu wachache.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilitaja wanaotakiwa kujiuzulu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyepewa sh bilioni 1.6 kutoka kwa mmoja wa wamiliki wa IPTL, James Rugemalila.
Mapendekezo hayo yalitolewa baada ya Kamati hiyo kupewa taarifa fupi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe.
PAC inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ndiyo iliyopewa kazi ya kupitia ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serrikali (CAG) ambayo sasa iko tayari kuwasilishwa bungeni kujadiliwa.
Watuhimiwa wengine katika kashfa hiyo iliyosababisha wahisani kusitisha misaada yake nchini ya zaidi ya sh trilioni moja ni Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndullu, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Felchesmi  Mramba, huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitajwa kuhusika kutokana na uzembe wa watendaji wake.
Mapendekezo hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha wabunge wa CCM, kinachotarajia kufanyika leo mjini hapa
Habari kutoka ndani ya wabunge wa CCM, zilisema kuwa mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, atawasilisha taarifa fupi ya kamati yake kuhusu kashfa hiyo ili kutoa mwelekeo kwa wabunge hao kuchangia mjadala wa ripoti ya uchunguzi ya CAG, itakapowasilishwa Bungeni wiki ijao.
Ndugai alaumiwa
Baadhi ya mawaziri na makada wa CCM, wamemlaumu Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, kwa kuruhusu mjadala wa wiki iliyopita ambapo baadhi ya wabunge kuishambulia mahakama na serikali
Hata hivyo jana Ndugai alisema haoni kama alifanya kosa bali alikuwa akitaka ushauri wa kuliendesha jambo hilo baada ya kuombwa muongozo wa kuwapo kwa barua ya mahakama inayozuia Bunge lisijadili suala la Escrow
“Ni kweli nimepata lawama kutoka kwa baadhi ya watu lakini mimi nilifanya vile kwa nia njema kwakuwa jambo lenyewe lilikuwa zito sana” alisema
 IPTL yatia doa mbio za Pinda
Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa kashfa ya IPTL, imetoa doa  harakati za Waziri Mkuu Mizengo Pinda,  kuwania urais mwakani.
Pinda ambaye hatajwi kuhusika  moja kwa moja na kashfa hiyo, lakini anaguswa na uzembe wa watendaji wake, wiki hii alikuwa na wakati mgumu kiasi cha kuzomewa na wabunge.
Pinda alizomewa bungeni pale alipojaribu kuitetea ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Akaunti Escrow isijadiliwe bungeni kwa madai kuwa kuna kesi zaidi ya 10 zinazohusu IPTL na wadau wake hivyo kujadili ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Duru za siasa ndani na nje ya Bunge, zinaeleza kuwa kwa jinsi hali ilivyo kashfa hiyo haiwezi kumuacha Pinda salama na hali ikiwa hivyo harakati zake za kutaka kuwania urais kimyakimya,  zitakuwa zimekwisha au kupata dosari kubwa.
Wadadavuzi wa mambo ya siasa, wameliambia Tanzania Daima Jumapili, nguzo kubwa ya Pinda katika kuwania urais ni usafi wake kwani hana kashfa wala makando kando ya ufisadi ukilinganisha na baadhi ya makada  wanaotajwa ndani ya CCM.
“Ukimsimamisha Pinda na Lowassa na Membe, Lowassa alichafukachafuka kwa kashfa za ufisadi ambazo baadaye zimeonekana sio za kweli. Membe naye alishachafuka. Pinda hana makandokando, na hiyo ndiyo nguzo yake kuu ya kuwania urais. Sasa hii ndio kashfa yake ya kwanza na kibaya zaidi imekuja wakati wa joto la urais na yeye anautaka,” alisema waziri mmoja jina limehifadhiwa.
Kutokana na hali hiyo, Pinda ni miongoni mwa viongozi wa juu wa serikali wasiotaka ripoti ya uchunguzi wa kashfa hiyo, iende bungeni kwani madhara yake ni makubwa kwa serikali na kwake
Wakati akichangia kwenye mjadala wa Escrow Akaunti uliotikisa Bunge wiki, bila hata kusoma alama za nyakati kwa wabunge, Pinda alisema kwa hatua iliyofikia, Bunge linahitaji utulivu na busara zaidi katika kufanya maamuzi.
Alisema mihimili mitatu, iliyopo  yaani Bunge, Mahakama na Serikali  kwa mujibu wa katiba na kila chombo kimepewa eneo lake la kusimamia na namna ya kuendesha shughuli zake,
“Mheshimiwa Spika, Naibu Spika nimeona nisimame niseme jambo kwa ufupi sana, rai yangu kwako na kwa wabunge mnapofika katika hatua ambazo mnataka kidogo utulivu mnataka hekima kubwa ni pale mnapofika hatua kama hii niliyoiona leo.
“Nimeogopa sana kwa baadhi ya kauli zilizotoka kujaribu kuona mahakama kama ni chombo kilichotumika kujaribu kuficha uozo, nadhani si kauli nzuri sana hasa sinapotoka kwenye muhimili kama huu, umepata michango kutoka kwa wabunge na mimi ni mmoja wapo ambaye ningependa haya mambo yaishe lakini lazima tukubali kwamba katika kufanya jambo hili ni lazima tutumie busara kubwa kuhakikisha kwamba maamuzi mtakayoyafanya yawe ni maamuzi ambayo hayataleta ghasia za muingiliano wa majukumu ya chombo kingine chochote,” alisema na kusababisha kuzomewa
Mbali ya Pinda kujitahidi kuepusha mjadala wa ripoti ya CAG isiingie bungeni, baadhi ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamepanga kumtetea Pinda asiwajibike kwa makosa ya watendaji wake.
Wakati kundi hilo likiendesha kampeni hizo, kundi linguine ambalo ni kubwa limejipanga kumshughulikia Pinda kwa hoja kwamba kama Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa aliwajibika kwa makosa ya watendaji wake, kwanini Pinda naye akafuata mkondo huo.
Harakati za kuzima kashfa hiyo isifike Bungeni, imepata kufanywa pia na Ikulu kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kwamba ripoti hiyo haijakamilika na kuwataka wabunge waache kushinikiza iende Bungeni.
Mgogoro uliosababisha fedha kuwekwa katika akaunti hiyo ya Tegeta ya BoT ulitokana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugoma kulipa gharama za uwekaji mitambo (Capacity Charge) kwa IPTL mwaka 2006 kwa vile ilibainika IPTL ilikuwa ikitoza gharama kubwa kuliko iliyopaswa.
Akaunti hiyo ya Tegeta ilianzishwa kwa sababu ya kuhifadhi fedha zote zilizopaswa kulipwa na Tanesco hadi hapo mgogoro baina ya pande hizo mbili umalizike.
Hata hivyo, Septemba mwaka jana, serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliagiza BoT kulipa fedha hizo kwa kampuni ya PAP mara baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema kwamba mgogoro baina ya wamiliki wa IPTL na Tanesco umemalizika na hivyo Benki Kuu haina sababu ya kuhifadhi fedha hizo.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post