Dar es Salaam. Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Tundu Lissu amemtaja Rais Jakaya Kikwete kuwa sehemu ya mgogoro mzima
wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL tangu ilipoingia nchini mwaka 1994.
Akichangia Ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC), Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema
ilijulikana miaka 20 iliyopita kwamba IPTL itakuja kuwaumiza
Watanzania.
“Mwaka 1994 wakati IPTL wanaandika MoU
(makubaliano ya awali) na Serikali, Waziri wa Nishati na Madini alikuwa
Kanali Jakaya Kikwete, mwaka 1995 wakati mkataba wa kununua umeme
unasainiwa kati ya Serikali na wawekezaji hawa, Waziri wa Fedha alikuwa
mtu aitwaye, Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.
“Miaka 20 baadaye Sh321 bilioni za Watanzania
zimeibiwa, Rais wa Tanzania ni Jakaya Mrisho Kikwete, tunataka fedha
zetu zirudi,” alisema Lissu.
Mara baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alisimama na kuomba
mwongozo kuhusu matumizi ya jina la rais bungeni.
Akisoma vifungu vya mwongozo wake, Nagu alisema
mbunge hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa
madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kwa madhumuni fulani na mbunge
hataweza kuzungumzia mwenendo wa Rais, jaji, spika au mtu yeyote hadi
pale kukiwa na hoja husika.
“Hivi kweli humu ndani lazima tuitane wezi au
kutumia lugha za maudhi? Lazima humu ndani tutumie lugha za staha na
tukafikia uamuzi utakaoheshimika na watu wote,” alisema Nagu.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliyekuwa
akiendesha kikao cha jioni alisema: “Nakubaliana na hoja ya waziri ni
kweli kanuni zinatuzuia kutumia maneno ya watu vibaya, tusitumie majina
ya Rais, mahakimu, majaji au majina yoyote.
Akihitimisha mchango wake, Lissu alisema:
“Sijatumia jina la Rais vibaya, ila nilichosema ni ukweli mtupu kuwa
kipindi wanakuja (IPTL) Rais wetu alikuwa waziri wa nishati, wakati
wanasaini makubaliano alikuwa waziri wa fedha na wakati fedha zinachotwa
Rais wetu ni Kikwete.”
Akizungumzia sakata hilo Lissu alisema: “Ni aibu
waziri kupewa Sh1.6 bilioni... hakuna jambo baya kama mwanasheria mkuu
wa zamani kupewa hongo ya Sh1.6 bilioni, hakuna jambo baya viongozi wetu
wa dini kupewa hongo, sasa sisi tunazungumza mambo mabaya yanayotokea,
hakuna mambo mabaya kama hakimu, jaji kupewa Sh400 milioni sehemu ambako
kesi ilikaa kwa muda mrefu na hakuna jambo baya kama fedha kuibiwa,”
alisema Lissu.
Kuhusu fedha hizo ni mali ya nani, Lissu alisema:
“Fedha hizi ni za wananchi na nchi hii, TRA (Mamlaka ya Mapato
Tanzania), CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) wote
wamesema ni fedha za umma, Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa) wamesema ni fedha za umma lakini watu pekee wanaosema siyo fedha
za umma ni wale waliokula.
“Mpaka majaji, viongozi wa umma, viongozi wa dini,
wanasiasa wamegawana, tunaambiwa katika mifuko... lazima watu
wawajibike kwa hili. Tuanze na hawa tunaowaweza ambao ni Waziri Mkuu
(Mizengo Pinda), Mwanasheria Mkuu (Frederick Werema), Tibaijuka (Profesa
Anna, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Chenge (Mbunge
wa Bariadi, Andrew), Ngeleja (Mbunge wa Sengerema, William) yaani majizi
yote yaliyomo humu tuyawajibishe,” alisema Lissu.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment