Dar/Z’bar/mikoani. Siku moja baada ya Kamati ya PAC kuweka
hadharani uchunguzi wa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, watu wa kada mbalimbali
wamependekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Zanzibar
Viongozi wa upinzani Zanzibar wamesema wote
waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ufisadi kupitia Akaunti ya Tegeta
Escrow wafukuzwe pamoja na kufunguliwa mashtaka badala ya kuendelea
kusubiri msimamo wa Rais katika jambo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Viongozi wa
Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na Tadea walisema kiwango cha fedha
kilichoibiwa ni kikubwa na haikubaliki kwa nchi inayoheshimu misingi ya
utawala bora.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Zanzibar, Ambar
Khamis Haji alisema viongozi walioguswa na ripoti ya uchunguzi lazima
wawe watu waugwana waondoke katika nyadhifa zao wenyewe wasubiri sheria
ichukuliwe mkondo wake.
Alisema pamoja na viongozi wa dini na majaji
walioguswa katika kashfa ni wakati mwafaka na wao kujiuzulu kutokana na
kitendo chao cha kudhalilisha mamlaka wanazoziongoza wakati wao
wanatakiwa kuwa mfano bora katika jamii. “Pamoja na kwamba fedha za
sadaka huwa hazichagui fedha halali au chafu hatuamini kama zilikuwa za
kanisa kutokana na kutumika kwa akaunti ya mtu binafsi,” alisema Ambar.
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa
CUF, Salim Bimani Abdallah alisema Serikali nzima inapaswa kujiuzulu
kutokana na ukubwa wa kashfa.
“Rais wetu ni mtendaji siyo kama mfalme,
haiwezekani kufanyike wizi mkubwa kama huo bila ya kufahamu na kuchukua
hatua mapema, Serikali nzima ivunjwe kuitishwe uchaguzi,” alisema
Bimani.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Issa Mohamed
alisema wakati umefika kwa wananchi kujifundisha na kuwa makini
wanapofanya uamuzi ya viongozi kwa sababu CCM imeshindwa kupambana na
vitendo vya ufisadi katika Serikali yake.
Alisema inasikitisha, wakati Sh306 bilioni zikipotea, wananchi wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kuanguka huduma za jamii.
“Dawa hakuna wanafunzi wanasoma chini ya sakafu
huku wengine wakikosa mikopo ya elimu ya juu, wazazi wakilazwa chini
kutokana na uhaba wa vitanda hospitali za Serikali.
“Katika misingi ya utawala bora wanahitajika
kujiuzulu kabla ya kufukuzwa na Rais ili sheria ichukue mkondo wake na
mali zao zitaifishwe,” alisema Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment