Katibu Mkuu wa CUF akipandisha bendera baada ya kuzindua tawi la Ufukoni Stand, Kata ya Ufukoni mjini Mtwara
Na Khamis Haji, Mtwara
Katibu Mkuu wa Chama
Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema ushirikiano wa
vyama vinne vya upinzani (Ukawa) ndio jibu sahihi kwa wananchi wengi
waliokuwa wakihoji iwapo CCM itang’olewa nani atachukua nafasi hiyo na
kukamilisha ndoto za Watanzania kuwa na maisha mazuri.
Maalim Seif amesema
hayo wakati akihutubia mikutano ya hadhara, akiwa katika ziara ya
kichama mkoani Mtwara, ambapo amekuwa akizindua matawi mapya ya CUF na
kuhimiza wananchi kujiandikisha katika daftari la kura na kushiriki
uchaguzi wa Serikali za mitaa Disemba 14 mwaka huu kukiweka upande CCM.
Katibu Mkuu wa CUF
amesema kwa miaka mingi wananchi walikuwa wakijiuliza nani atachukua
nafasi ya CCM kuongoza dola, lakini sasa wananchi hawana hofu tena baada
ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR Mageuzi na NLD kuamua kushirikiana
kukiondoa madarakani CCM.
Amesema CCM baada ya
kuongoza nchi kwa miaka 53 tokea uhuru kimeshachoka na hakina jipya tena
kinaloweza kuwafanyia wananchi na kimebaki kuonesha kibri na utawala wa
mabavu dhidi ya wananchi.
Amewataka wananchi
wasidanganyike kuwa CCM inaweza kutoa mgombea bora wa Urais kwa sababu
viongozi wote wa CCM wanafuata mfumo mmoja wa chama chao ambao kwa sasa
hauwezi kuwaletea mabadiko ya msingi wananchi wa Tanzania.
“Wala msidanganywe na
Rais Kikwete kuwa atakuja mtu mwengine kutoka CCM ambaye atakuleteeni
maendeleo, CCM waje na mgombea kama hariri lakini chini ya mfumo wao
hataweza kufanya kitu chochote kipya”, amesema.
Akizindua baada ya
kuzindua tawi jipya la CUF Kata ya Ufukoni, Manispaa ya Mtwara, Maalim
Seif amesema wananchi wamechoka kwa bakora za CCM.
Amesema sera za CCM
zimewadhoofisha wananchi walio wengi hasa vijana kiasi kwamba vijana
wengi wanaonekana ni wazee na unatamani kuwaamkia kutokana na maisha
duni chini ya sera za CCM.
“Nyinyi hapa Mtwara
sio wageni na hilo nahikaka bakora za CCM zimewatosha tuungane kuiondoa
madarakani CCM na kwa hili chini ya ushirikiano tuliouanzisha, CCM
itang’oka tu”, amesema Katibu Mkuu wa CUF.
Maalim Seif amesema
kazi iliyo mbele ya wananchi hivi sasa ni kujitokeza kwa wingi kwenda
kujiandikisha katika zoezi linaloendelea ili waweze kushiriki kikamilifu
katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi ujao na kukipa salamu CCM
muda wao wa kuondoka umefika.
Naibu Mkurugenzi wa
Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya amesema kama
kuna watu wanapaswa kupelekewa magari ya deraya na kuadhibiwa ni
viongozi wa CCM wanaochota fedha za wananchi kwa njia ya ufisadi na sio
wananchi wa Mtwara.
Kambaya amesema hivi
sasa taifa liko njia panda na kamwe wananchi hawawezi kunyamaza kutokana
na wizi na ufisadi unaofanywa ambao unasababisha madhara makubwa kwa
wananchi wanyonge.
“Hiki ni chama
kisichotekeleza ahadi, katika awamu hii walisema watashughulikia hali
mbaya magerezani, matatizo ya hospitali ya Muhimbili, wauza dawa za
kulevya, rushwa mahakamni na baadaye wakaahidi Katiba mpya, yote
hayakutekelezwa”, alisema Kambaya
إرسال تعليق