Dodoma. Ripoti ya sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200
milioni katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyotua bungeni wiki iliyopita,
imeibua mambo mazito baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kugundua kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti
hiyo zilikuwa mali ya Tanesco.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa
fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya
Tanesco kwa IPTL ni Sh321 bilioni, hivyo fedha zote za Escrow zilipaswa
kwenda Tanesco na bado ingekuwa inadai.
Ukaguzi wa akaunti hiyo uliamuliwa na Serikali
baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kudai
kuna ufisadi katika uchotaji wa fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro
wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni
ya kufua umeme ya IPTL.
Katika mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia
kiwango cha fedha ilichokuwa inalipa kwa gharama za uwekezaji kwa IPTL,
ndipo ikaamuliwa na mahakama ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa
inalipa ziendelee kuwekwa huko hadi mgogoro utakapokwisha.
Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na IPTL.
Baada ya ripoti ya uchunguzi huo kukabidhiwa
bungeni wiki iliyopita chanzo chetu kimeeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti
hiyo fedha ni za umma na zilipaswa kwenda Tanesco na shirika hilo
kuendelea kuidai IPTL Sh15 bilioni.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Kampuni ya PAP
haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za Kampuni ya Mechmar katika
IPTL kwani zilizuiliwa na mahakama, hivyo hawana hati halisi ya hisa na
kwamba ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za
uongo kuwa walinunua hisa kwa Sh6 milioni badala ya Dola za Marekani 20
milioni, hivyo kuikosesha Serikali Sh8.7 bilioni.
Pia imeeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
alivunja sheria kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye
gharama za uwekezaji isilipwe na hivyo kusababisha Serikali kupoteza
mapato ya Sh21 bilioni.
“Wizara ya Nishati na Madini haikufanya uchunguzi
wa awali (due diligence) kuhusu uhalali wa umiliki wa Kampuni ya IPTL na
ilisaini kutoa fedha bila ya kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi na
hivyo kusababisha kulipotezea Shirika zaidi ya Sh321 bilioni,” chanzo
chetu kilieleza.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa
juzi baada ya kutoka kwenye Kamati ya Uongozi, bila kufafanua alisema
ripoti itawasilishwa bungeni Novemba 26, mwaka huu kama ilivyopangwa na
kuwa angetoa taarifa ya kilichojiri kwenye Kamati ya Uongozi bungeni
leo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wameeleza
kuwa, wamekubaliana ripoti hiyo iwasilishwe kama ilivyopangwa na kwamba
muda huu ofisi ya Katibu wa Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
waipitie kwa ajili ya uwasilishwaji
- Mwananchi
Post a Comment