![](http://www.thisday.co.tz/media/picture/large/Mwakyembe.jpg)
Mpango huo unaosukwa kwa siri
kubwa chini ya mkataba unaopendekezwa; imebainika kuwa kisheria ni
mbovu, hauna maslahi kwa taifa na unahatarisha usalama wa Tanzania.
*Wajiandaa kuuza haki za kuiendesha kwa bei ya kutupa
*Wathamanisha ardhi, maji Sh milioni 246 kwa miaka 33
*Thamani halisi ni Sh bilioni 85, ni mkataba hatari kwa usalama
*Mwekezaji anapewa ‘bure’, TPA kukopa mtaji Sh bilioni 306
*Dk. Mwakyembe ahusishwa, Kigogo adaiwa kuhongwa bilioni 1
Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeingia katika kashfa nyingine
nzito kutokana na mpango wake wa siri inaoukamilisha wa kubinafsisha
mlango wa Bandari ya Dar es Salaam katika eneo liitwalo Gerezani Creek
kwa miaka 33 kuanzia mwaka huu.
Mkataba huo ulipaswa kutiwa
saini Septemba 6, mwaka huu, lakini inaelezwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, Joseph Simbakalia, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TPA, ameukataa.
![]() |
pichani niKaimu mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Mzee Maden Kipande |
Inaelezwa
kuwa Simbakalia aliwashawishi wajumbe wengine wa Bodi waukatae mkataba
huo kutokana na ubovu wake. Mkataba husika uliandaliwa kwa siri jijini
Geneva, Uswisi na baadhi ya vikao kufanyika Nairobi nchini Kenya, kisha
ukaletwa nchini kwa nia ya kutiwa saini bila kubadilishwa kwa njia
yoyote.
Eneo ‘linalogawiwa’ kwa Mzungu
mwekezaji, ni pamoja na Bandari ilikojenga jengo jipya la ghorofa 35,
ingawa wengine wanasema mchoro wa awali umebadilishwa na sasa litakuwa
na ghorofa 40.
Mpango ulivyosukwa
Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe, inadaiwa kwa kushikiana na Kaimu Mkurugenzi wa
Bandari, Mzee Madeni Kipande, walianzisha kwa siri mchakato wa
kubinafsisha mlango wa Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia eneo zinakotia
nanga ‘boti za kasi’ ziendazo Zanzibar hadi eneo yanakopakuliwa magari
kutoka ng’ambo.
Habari za uchunguzi zinaonesha
kuwa kampuni inayodaiwa kuwa inataka kubinafsishiwa eneo hili la
Bandari kwa miaka 33 imesajiliwa miezi michache iliyopita na hadi
Jumamosi Oktoba 18, mwaka huu kampuni hii ilikuwa haijaingizwa kwenye
orodha iliyopo kwenye tovuti ya Msajili wa Kampuni (Brela).
Mkataba unaitaja kampuni ya
Impala Terminals Tanzania Limited kuwa inamilikiwa na Kampuni ya
Vullstar Limited ya Bahamas, lakini uchunguzi uliofanywa na Chanzo
chetu, kampuni ya Vullstar haina wavuti na wala haionekani kwenye
mtandao wowote.
Visiwa vya Bahamas vinasifika
duniani kwa kuwa na kampuni feki, na hivi karibuni vilikuwa na kashfa ya
kuwa na nyumba moja inayoonekana kuwa ni ofisi ya kampuni zaidi ya
3,000; nyumba hiyo ikiwa na vyumba visivyozidi sita.
Ukiacha utata wa kampuni mpya
ya Impala kumilikiwa na Kampuni ya Vullstar isiyokuwapo kwenye mtandao
wa intaneti, kampuni ya Impala Terminals Tanzania Limited anwani ya
msingi inayoitumia hapa nchini ni ya simu ya mkononi ya airtel (namba
inahifadhiwa), ambayo inapokewa na mtu asiyejitambulisha kwa jina ila
ndiye ametajwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo kwenye mkataba
unaokusudiwa kusainiwa.
Alhamisi (Oktoba 16, 2014)
Chanzo hicho kilipowasiliana na Mkurugenzi huyo, asiyetajwa jina ila
yupo kwenye mkataba ambao Bandari inapaswa kukopa dola milioni 180 (Sh
bilioni 306) kuendesha mradi huu, alihoji: "Umeupata wapi mkataba huu?
Huu ni mkataba wa siri, uniambie aliyekupa mkataba huu ndipo nikujibu."
Mwandishi alipomwambia kuwa taaluma hairuhusu kutaja majina ya waliompa
mkataba, Mkurugenzi huyo akasema: "Andika maswali unitumie kwenye barua
pepe."
Mwandishi alimsomea anwani za
barua pepe zilizoko kwenye mkataba, naye akakiri kuwa ndizo; na akataka
maswali yatumwe kupitia barua pepe hizo.
Mwandishi aliandika maswali 11
na kumpelekea barua pepe mbili zilizopo kwenye mkataba, ambazo nazo ni
za kampuni nyingine iitwayo Impala Terminals, na badala ya maswali
kujibiwa; huyo Mkurugenzi mwenye namba ya airtel, Ijumaa Chanz chetu
haijaapata majibu kutoka kwa mtu mwingine kabisa aliyeko Geneva, Uswisi
akisema:
"Mpendwa Bwana Balile, asante kwa maswali yako kwa Impala. [Huwa] hatuzungumzii uvumi au hisia. Salaam za upendo, Victoria Dix."
Huyu Victoria Dix kwa mujibu wa mtandao wa www.impalaterminals.com ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano upande wa mashirika wa kampuni ambayo ina makao yake Geneva, Uswisi.
Mkataba unachotaka
Mkataba huo wenye shinikizo
kubwa kutoka kwa kigogo mmoja ndani ya Wizara ya Uchukuzi, ambaye
inadaiwa amehongwa dola 800,000 za Marekani (Sh bilioni 1.36) akamalizia
ununuzi wa kiwanja kutoka kwa Mjerumani mmoja karibu na eneo la Bahari
Beach Hotel, Dar es Salaam; unatajwa kuwa utahatarisha usalama wa taifa.
Masharti inayotoa kampuni ya
Impala Terminals Tanzania Limited, ni kuwa lazima Bandari ikubali
kuingia ubia na kampuni hiyo kwa kuunda kampuni ya pamoja inayotajwa kwa
Kiingereza na lugha ya kisheria kama Joint Venture Company (JVC),
ambayo kwa sasa haijasajiliwa kwa nia ya kuendesha Bandari chini ya
Ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Mtaji wa vitabuni, inaelezwa
kuwa kampuni itakayoundwa itakuwa na mtaji wa vitabuni wenye thamani ya
dola milioni 27 za Marekani utakaogawanywa katika hisa 10,000 kwa maana
kuwa kila hisa itakuwa na thamani ya dola 2.7.
Kampuni ya Impala Terminals
Tanzania limited inajinadi kuwa itabuni, itaendeleza, itatoa mtaji na
kuendesha Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga gati mbili katika eneo la
Gerezani Creek, ila wanatumia ujanja kwa kudai kuwa ni uwekezaji wa
pamoja na TPA.
Mbali na ujenzi wa gati mbili,
kampuni ya Impala inajinadi kuwa itatoa ajira kwa Watanzania na kuleta
nchini ujuzi wa uendeshaji bora wa bandari. Hata hivyo, kati ya maswali
waliyoulizwa na kukataa kuyajibu ni pamoja na ukweli kwamba kampuni hii
au Vullstar inaelezwa kuwa haijawahi kuendesha bandari yoyote duniani na
hivyo haina uwezo inaotamba kuwa nao.
Kampuni nyingine wanayotumia
anwani ya barua pepe zake, impalaterminals.com, kwenye mtandao inajinadi
kuwa inao uzoefu mkubwa katika sehemu mbalimbali duniani wa kutuza
maghala (warehouses) na si kuendesha bandari. JAMHURI haikuweza kufahamu
uhusiano uliopo kati ya Impala Terminals, Vullstar na Impala Terminals
Tanzania Limited.
Wakati mkataba huo unaizuia
Bandari kuhamishia hisa zake kwa mwekezaji mwingine wakati wote wa uhai
wa mkataba, yaani miaka 33; Impala wao wanaruhusiwa kuhamisha hisa zao
kwenda kampuni ya Vullstar bila kulazimika kuomba ruhusa kwa TPA.
Gharama ya mradi
Gharama ya mradi atakaopewa
mwekezaji huyu chini ya mkataba ni dola milioni180 za Marekani. Hata
hivyo, mkataba huu umeandikwa kwa ujanja wa hali ya juu. Kifungu cha
5.2.1 cha mkataba kinahamishia jukumu la kukopa mtaji kwa TPA na si kwa
mwekezaji kama ilivyoelezwa awali.
Kifungu hiki kinasema:
"Bandari ina wajibu wa kutoa asilimia 30 ya hisa kama mchango wake wa
ardhi na matumizi ya maji na mkopo wote wa wanahisa unaohitajika kwa
ajili ya kampuni (JVC) ambao si zaidi ya Mtaji wa Kuanzishia Mradi (dola
milioni 180) na inaweza pia kulipia hisa asilimia 19 kwa njia ya fedha
kama mchango wake kwa JVC."
Kifungu cha 5.1.1 kinasema
Impala Tanzania Terminals Limited yenyewe itamiliki hisa asilimia 51 na
wanatumia maneno kuwa itatafuta mkopo kwa ajili ya hisa hizo na nyingine
kadri itakavyohitajika. Maana yake ni kwamba Impala haitawekeza kitu na
bado itamiliki asilimia 51 ya hisa kwenye kampuni hii kwani Mtaji wa
Kuanzia ambao ni dola milioni 180 za Marekani umetajwa wazi kuwa
utakopwa na TPA.
Thamani ya hisa na ardhi
Maajabu mengine katika mkataba
huo, thamani ya hisa zinazopendekezwa kumilikiwa na Bandari bei yake
iko chini ukilinganisha na zinazopendekezwa kumilikiwa na Impala.
Bandari wanatajwa kuwa
watapewa ‘bure’ asilimia 30 ya hisa; sawa na hisa 55 kama mchango wao wa
haki ya kumiliki ardhi na maji ilipo Bandari ya Dar es Salaam, kisha
watapaswa kulipia hisa 36 kwa gharama ya dola 95,000 za Marekani kwa
hisa zitakazotolewa na JVC. Wao impala watachukua hisa 94 kwenye JVC kwa
gharama ya dola 255,000 za Marekani.
Sambamba na malipo hayo,
Bandari pia watapaswa kutoa mkopo wa dola 855,000 za Marekani huku
Impala mkataba ukiwataka watoe mkopo wa dola 2,295,000 za Marekani kwa
nia ya kuijengea uwezo wa kifedha kampuni itakayoundwa.
Maajabu yanayotokea ni kuwa
hisa zilizotolewa kwa Bandari thamani yake inakuwa dola 2,638.88 za
Marekani kwa kila hisa, wakati hisa zilizotolewa kwa Impala thamani yake
ni dola 2,684.21 za Marekani kwa kila hisa. Utofauti huu wa thamani ya
hisa haukuelezwa umetokana na nini. Kwa mantiki hiyo, asilimia 30 ya
hisa zilizotolewa kwa Bandari kwa njia ya ardhi ina maana ardhi hiyo
imethamanishwa kuwa ni dola 145,000 (Sh milioni 246).
Suala la ardhi ndio kilio cha
wataalam. Vyanzo vya kuaminika kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya
Makazi, vimeliambia JAMHURI kuwa thamani ya eneo la Bandari wanalopanga
kubinafsisha ni zaidi ya dola milioni 50 za Marekani (Sh bilioni 85),
hivyo kulitoa kwa thamani ya Sh milioni 246 ni kuhujumu uchumi wa nchi.
Impala yatoa masharti magumu
Pamoja na kwamba haijasaini
mkataba huu, Impala imetoa masharti magumu kwa Serikali. Kupitia mkataba
huu inajipa mamlaka ya kuchunguza uwezo wa TPA kifedha na haki zote
zilizopata kutolewa kupitia mikataba mingine, na kupitia Kifungu cha 3
chote hakuna mahala ambako Bandari inapaswa kuichunguza Impala kuona
kama inao uwezo kifedha.
Kampuni hii inataka kukagua
masharti ya usafirishaji kati ya Bandari na TAZARA. Pia TPA inapaswa
kuikabidhi Impala nyaraka zilizotolewa na mamlaka halali zikiisamehe
kodi Impala. Inaitaka Bodi ya Wakurugenzi ya TPA kukasimisha madaraka
yake kwa Impala kwa maandishi juu ya uendeshaji wa Bandari kwa miaka
yote 33 kuwa haitaingilia utendaji wake wakati wowote.
Mkataba unataka Waziri wa
Fedha akabidhi barua ya kujifunga kuwa atahakikisha mkataba kati ya TPA
na Impala unatelekezwa bila kubadilishwa kwa kipindi chote cha miaka 33
na TPA kuikabidhi barua ya kuthibitisha kuwa Bandari haitabadilisha
matumizi ya ardhi au kuingia mkataba na mwendeshaji mwingine kwa muda
wote wa miaka 33 ya mkataba.
Masharti magumu yanahitimishwa
kwa kifungu cha 3.5 chenye kusema kuwa ikiwa TPA itashindwa kutimiza
masharti hayo ndani ya miezi mitatu tangu siku ya kusainiwa kwa mkataba,
basi mkataba utakuwa umevunjika. Ingawa kwenye eneo hili wanasema
hakuna atakayedaiwa gharama za kuvunjwa kwa mkataba, kiujanja chini ya
kifungu cha 22.1.1 kinaelekeza TPA idaiwe.
Kifungu hiki na kinachofuata
cha 22.1.2 vyote vinasema ikiwa mkataba huu utavunjika iwe makosa
yamefanywa na Impala au Bandari, basi TPA ndiye atakayelipa gharama za
kuvunjika kwa mkataba huu kwa Impala. Mbaya zaidi, mkataba unasema ikiwa
Bandari itashindwa kulipa, basi Serikali ndio itapaswa kulipa deni
husika au mali za Serikali zitakamatwa kokote duniani.
Kundoshwa kwa mamlaka ya dola (waver of sovereignty immunity)
Mkataba unapendekeza chini ya
Kifungu cha 34 kwa tafsiri isiyo rasimu unasema: "[Bandari] inaridhia
kwa ujumla suala lolote kuhusu mashitaka au nafuu inayotolewa [kwa
Impala] dhidi yake [TPA] kwa njia ya zuio au amri ya kutekeleza jambo
maalum au kupata kitu chochote kiwacho na mali zake kuwa wazi kwa ajili
ya utekelezaji wa amri au hukumu au mchakato unaoendeshwa kuhusu mali
yoyote [ya TPA au Serikali].
"Kinga inaondolewa kwa ujumla
wake bila haki ya kuirejesha dhidi ya mashitaka na mwenendo wake na
utekelezaji au kukamata mali (ikiwa ni pamoja na hukumu za awali na
ukamataji kwa msaada) ambako kuanzia sasa haki hii inaweza kurejeshwa tu
kwa mujibu wa sheria za mamlaka yoyote na inatamkwa kwamba kundolewa
kwa kinga ya mashitaka kutatekelezwa kwa kiwango kinachoruhusiwa na
sheria."
Kuna taratibu za kisheria mtu
au taasisi yoyote inapotaka kuishitaki Serikali, lakini kwa mkataba huu,
Impala inataka Serikali iwe wazi kushitakiwa wakati wowote
itakapojisikia kufanya hivyo bila kuomba kibali chochote. Kwa sasa
kuishitaki Serikali inapaswa kutolewa notisi ya siku 90, kitu
wasichokitaka Impala.
Nafasi ya Watanzania
Katika mkataba huo, Watanzania
wanapewa kazi za ukiranja. Mkataba unapendekeza Bodi ya Wakurugenzi
Watano, na Impala ambaye hakukopa mtaji ndiye awe na Wakurugenzi watatu,
huku Bandari waliokopa mtaji na kutoa haki ya kutumia ardhi na maji
wakitakiwa kuwa na wakurugenzi wawili kwenye Bodi hiyo.
Katika nafasi za utendaji,
inapendekezwa Afisa Mtendaji Mkuu atoke kwa Impala, Afisa Fedha Mkuu
atoke Impala na Afisa Uendeshaji Mkuu naye atoke Impala. Kwa upande wa
Tanzania inapendekezwa Mtanzania awe Naibu Mtendaji Mkuu
(anayeshughulikia uhusiano) na mwingine awe Afisa Utumishi na Rasilimali
Watu.
Mkataba huu unaopendekezwa una
upungufu mkubwa, likiwamo pendekezo kwamba mbia atakayeshindwa kulipia
hisa, zilipiwe na mwenzake na hivyo kuhamisha umiliki wa hisa kama
ilivyotokea kwa Benki ya NBC ambako mwekezaji sasa anaimiliki karibu kwa
asilimia 100.
Mwakyembe, Kipande wakaa kimya
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe pamoja na kupelekewa maswali ofisini kwake na kupelekewa ujumbe wa simu ya mkononi, hakujibu.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande amegoma kuruhusu mwandishi
kuingia ofisini kwake na hata alipopigiwa simu hakupokea, lakini
alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu akajibu kwa kusema: "Tutawasiliana
baada ya kesi kukamilika."
Mwaka huu, Kipande
alilifungulia JAMHURI kesi Mahakama Kuu ya Tanzania na kupata hukumu ya
awali inayolizuia gazeti hili kuandika habari zisizo za kweli dhidi ya
Kipande hadi kesi ya msingi iishe. Kati ya mambo aliyolalamikia Kipande
katika kesi hiyo ni pamoja na habari kwamba Bandari ya Dar es Salaam
haina kamera za usalama (CCTV).
Ikiwa mkataba huu utapitishwa,
basi Serikali haitakuwa na uwezo wa kuingia katika eneo la Bandari bila
ruhusa ya Impala au kubadili matumizi kwa miaka 33 hadi Impala iwe
imeridhia mabadiliko hayo iwapo tu yanatimiza masilahi ya kampuni hiyo.
Chanzo: GAZETI LA JAMHURI
Post a Comment