Madudu zaidi meno ya tembo

Dar es Salaam. Wakati maofisa wa Serikali za Tanzania na China wakipuuza tuhuma zinazohusisha ziara ya Rais wa China, Xi Jinping na utoroshaji wa meno ya tembo, ripoti hiyo imeanika madudu mengi ikionyesha jinsi nyara hizo zinavyotoroshwa nchini.
Juzi taasisi iitwayo Environmental Investigation Agency (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira– EIA) ilitoa hadharani ripoti ambayo inataja maofisa na wanausalama wa China kwamba walitumia fursa ya kidiplomasia kusafirisha meno ya tembo kwa ndege ya Rais Jinping ambaye alitembelea Tanzania Machi 2013.
Ikulu ya Dar es Salaam na Ofisi ya Mambo ya Nje ya China kwa nyakati tofauti zilisema taarifa hizi siyo za kweli na jana Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ilitoa taarifa bungeni na kuziita taarifa hizo kuwa ni za “kupikwa”.
Wakati hayo yakiendelea, ripoti hiyo ya EIA iliyopewa jina la Vanishing Point: Criminality, Corruption and Devastation of Tanzania’s Elephants (Hatua ya kutoweka: Uhalifu, Rushwa na Kuangamizwa kwa tembo wa Tanzania), inafichua madudu zaidi yanayoweka bayana jinsi uhalifu wa utoroshaji wa meno ya tembo unavyofanyika.
Ripoti hiyo inalitaja pori la akiba la Selous kuwa kituo cha mauaji ya tembo, kwani matukio ya ujangili hupangwa katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo, kisha kutekelezwa kwa msaada wa polisi na baadhi ya wananchi.
Inavitaja vijiji vilivyopo katika maeneo ya Mloka, Tunduru, Namtumbo, Liwale na Kilwa ambako wafanyabiashara wadogo kutoka Dar es Salaam hukodishwa silaha na wawindaji, kisha kuingia katika hifadhi hiyo na kufanya uhalifu.
“Wakati mwingine wawindaji kutoka nje ya eneo hilo hutumiwa na baadhi ya maofisa kutoka serikalini,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Katika tukio la aina yake, ripoti hiyo imeeleza tukio la katikati ya mwaka huu ambapo kundi la wawindaji kutoka Arusha lilitumwa na maofisa wa polisi waliokuwa Mloka na kuingia katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kuwinda.
Inadaiwa kuwa maofisa hao wa polisi walitoa silaha kwa kundi hilo la wawindaji na baada tu ya mauaji ya tembo wapatao watano walichukua meno kutoka kwa wawindaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tembo akishauawa, meno yake hukatwa kisha kufukiwa hadi pale mnunuzi anapowasili ambapo hufukuliwa na kupewa.
EIA katika ripoti hiyo inabainisha kuwa meno mengi ya tembo kutoka Selous husafirishwa kwenda Dar es Salaam, ama kwa kutumia barabara kwa maana ya magari ambayo yametengezwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo, au kwa kupitia majini wakitumia mitumbwi ya asili.
“Wakati mwingine pikipiki hutumika kupitia njia za vichakani kukusanya meno hayo kule ambako zimefichwa hadi kufikia barabara kuu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo. Kutoka kwenye njia kuu husafirishwa kwa magari binafsi ambayo yanakuwa sehemu maalumu kwa ajili ya kuficha pembe hizo au kupitia mabasi ambayo husafirisha meno ya tembo zaidi kuliko abiria kutokana na malipo makubwa ambayo hutolewa kwa kazi hiyo.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post