Chawata: Hatupo tayari kurubuniwa na wanasiasa

Mwenyekiti wa Chawata, John MlabuWATU wenye ulemavu wamesema kuwa hawapo tayari kushawishiwa na kutumiwa na wanasiasa katika suala la upigaji wa kura ya maoni bali watahakikisha wanasoma na kuelewa Katiba inayopendekezwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jarida la watu wenye ulemavu ‘sauti ya siti’ lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Mwenyekiti wa Chawata, John Mlabu alisema kuwa nia yao sio kuwa na serikali nyingi bali kuwa na Katiba inayosaidia kundi hilo.
Mlabu alisema kuwa walemavu ni lazima wahakikishe wanapiga kura kwa maslai yao baada ya kusoma Katiba hiyo na kuona iwapo kuna masuala yanayowagusa moja kwa moja.
“Tusikubali kupiga kura kwa kusukumwa na wanasiasa ila tupige tukiamini katika yale yanayotugusa sio wingi wa serikali zinazosemwa,” alisema.
Alisema kuwa ni muhimu wafadhili wakasaidia kundi hilo liweze kupata nakala za Katiba inayopendekezwa ili kila mmoja aelewe kilichoandikwa katika Katiba hiyo.
Naye Katibu wa Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), Stella Jailos alisema kuwa kipindi hiki ni lazima walemavu wawe makini kwani yapo makundi mbalimbali yatakayohitaji kuwatumia kwa maslai yao binafsi.
Jailos alisema, kuwa ni vyema makundi mbalimbali katika jamii yakawasaidia walemavu kuijua na kuisoma Katiba inayopendekezwa ili waweze kushiriki kupiga kura kwa haki.
“Sisi hatujabahatika kuiona wala kuisoma Katiba inayopendekezwa hivyo ni vyema tukawa makini tutakapopata kuhakikisha tunasoma na kuelewa ili kura yetu tuweze kutoa kwa haki,” alisema.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki aliipongeza Tamwa pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu, (UNFPA) nchini kutokana na kufadhili jarida hilo litakalosaidia walemavu kutambua haki yao.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post