WATU
wenye ulemavu wamesema kuwa hawapo tayari kushawishiwa na kutumiwa na
wanasiasa katika suala la upigaji wa kura ya maoni bali watahakikisha
wanasoma na kuelewa Katiba inayopendekezwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jarida la
watu wenye ulemavu ‘sauti ya siti’ lililoandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Mwenyekiti wa Chawata, John Mlabu
alisema kuwa nia yao sio kuwa na serikali nyingi bali kuwa na Katiba
inayosaidia kundi hilo.
Mlabu alisema kuwa walemavu ni lazima wahakikishe wanapiga kura kwa
maslai yao baada ya kusoma Katiba hiyo na kuona iwapo kuna masuala
yanayowagusa moja kwa moja.
“Tusikubali kupiga kura kwa kusukumwa na wanasiasa ila tupige
tukiamini katika yale yanayotugusa sio wingi wa serikali zinazosemwa,”
alisema.
Alisema kuwa ni muhimu wafadhili wakasaidia kundi hilo liweze kupata
nakala za Katiba inayopendekezwa ili kila mmoja aelewe kilichoandikwa
katika Katiba hiyo.
Naye Katibu wa Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta),
Stella Jailos alisema kuwa kipindi hiki ni lazima walemavu wawe makini
kwani yapo makundi mbalimbali yatakayohitaji kuwatumia kwa maslai yao
binafsi.
Jailos alisema, kuwa ni vyema makundi mbalimbali katika jamii
yakawasaidia walemavu kuijua na kuisoma Katiba inayopendekezwa ili
waweze kushiriki kupiga kura kwa haki.
“Sisi hatujabahatika kuiona wala kuisoma Katiba inayopendekezwa hivyo
ni vyema tukawa makini tutakapopata kuhakikisha tunasoma na kuelewa ili
kura yetu tuweze kutoa kwa haki,” alisema.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki aliipongeza
Tamwa pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Idadi ya
Watu, (UNFPA) nchini kutokana na kufadhili jarida hilo litakalosaidia
walemavu kutambua haki yao.
- Tanzania Daima
إرسال تعليق