MBUNGE
wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), ameliomba Bunge kubadilisha kanuni
ili Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi Christopher Chiza, achapwe
viboko bungeni akamuonyeshe mkewe.
Filikunjombe, alisema kanuni hiyo iruhusu mawaziri wote wanaoshindwa
kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha, wachapwe viboko na kutolea mfano
wa Waziri Chiza kwamba, alipaswa kuchapwa viboko kwa kushindwa kujibu
swali la Mbunge wa Mwibara, Kange Ligola (CCM), juzi.
Akiomba mwongozo wa Spika jana bungeni baada ya kipindi cha maswali
na majibu, Filikunjombe, alisema Waziri Chiza mwenye dhamana ya kilimo,
jana alishindwa kujibu swali la Ligola na badala yake aliishia kutoa
maneno ya kejeli kwa Mbunge huyo.
“Jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Waziri Chiza
alishindwa kabisa kujibu swali la Ligola aliyetaka Serikali kutoa kauli
juu ya mazao ya wakulima yaliyonunuliwa kwa mkopo na yale ambayo
hajanunuliwa na yako kwenye hatari ya kuharibika wakati wa msimu wa
mvua…
“Badala ya kujibu swali hili, Mheshimiwa Waziri aliishia kutoa maneno
ya kejeli kwa Ligola kwamba yeye anayeshindwa kuelewa ndiye mzigo…
“Mwalimu Nyerere alisema wakati wa utawala wao hawakuwa na mswalia
mtume kwa wala rushwa, maana hawakumuachia hakimu kuhukumu, kwani
walikuwa wanawachapa viboko sita wakati wa kuingia na sita wakati wa
kutoka wakawaonyeshe wake zao.
“Na sisi tusiwe na mswalia mtume kwa mawaziri wanaoshindwa kujibu
maswali ya wabunge, tuwachape viboko bungeni wakawaonyeshe wake zao,”
alisema Filikunjombe na kuibua vicheko kwa wabunge ukumbini hapo,
akiwemo Chiza mwenyewe.
Katika swali lake la nyongeza juzi, Ligola alisema Waziri Chiza ni
mzigo, kwani ameshindwa kuwasaidia wakulima wa mahindi, mpunga, pamba na
mazao mengine ambao hawana uhakika wa soko na mazao yao yanaozea kwenye
maghala.
Alisema katika jimbo lake la Mwibara, baadhi ya wakulima wa mahindi
mazao yao yamekopwa na haijulikani watalipwa lini huku mazao mengine
yakikosa soko.
Akijibu swali hilo kwa jazba, Chiza alisema yeye sio mzigo bali Mbunge huyo ndiye mzigo kutokana na uelewa wake mdogo.
Chiza alitajwa kuwa mmoja wa mawaziri mizigo na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, wakati wa ziara zake mikoani ambako alishuhudia
kilio kikubwa cha wakulima huku wakilalamikia kwamba, hawajawahi kumwona
Waziri Chiza kwenda kusikiliza na kujionea matatizo yao.
إرسال تعليق