Jumapili iliyopita, tulijadili sehemu ya kwanza ya makala haya. Tuliangalia kwa muhtasari suala la Rais wetu kwenda kutibiwa nje ya nchi na kutoa taarifa kuwa utaratibu huo ni wa kawaida kwa marais na viongozi wengine hapa Afrika.
Tulitoa pole kwake, familia yake na Watanzania
wote na kujenga hoja iliyohoji umuhimu na utaratibu wa viongozi wengi wa
Afrika kuendelea kupata huduma bora za matibabu Ulaya na Marekani, huku
nchi zao huduma zake za afya zinatia hofu. Tuliangalia takwimu za
kimataifa juu ya masuala ya afya na kugusia Tanzania imesimamia wapi.
Tulionyesha kuwa Tanzania ikiamua kuboresha huduma
zake za afya ili kila mmoja, mwenye cheo na asiye nacho, aliye mbunge
na asiye mbunge na kadhalika, aweze kutibiwa hapa ndani ya nchi. Hilo
linawezekana. Tulitoa mfano wa fedha za umma zilizoibiwa katika akaunti
ya ESCROW Sh200 bilioni(wakati huo), sasa zikiwa Sh321 bilioni, baada ya
taarifa ya CAG kuonyesha hivyo na kusisitiza kuwa fedha hizo zingeweza
kabisa kututengenezea maelfu ya madaktari bingwa achilia mbali kama
tungeamua kuziwekeza katika maeneo mengine ili kuboresha sekta ya afya.
Leo tutaendelea kuangalia udhaifu mkubwa na wa
kimakusudi unaofanywa na Serikali yetu kwa jumla katika uboreshaji wa
sekta ya afya na kutoa suluhisho la kudumu.
Kikombe cha Babu Loliondo
Alipotokea mzee wa Loliondo, tulishuhudia viongozi
wakubwa wa Serikali wakikimbilia huko kwenda kunywa kikombe ili
waponywe magonjwa yao. Viongozi hao walifanya hata wananchi wa kawaida
waamini kuwa kikombe cha babu kinaponya, madege na misafari ya magari
kutoka kila kona ya nchi vikaelekezwa Loliondo. Loliondo ikawa Loliondo.
Watu wakawaondoa wagonjwa wao hospitalini ili wawapeleke Loliondo.
Loliondo ilikuwa ni Kigezo cha ujinga na upuuzi wetu, kilionyesha ni
namna gani tunaamini katika “tunguli na maajabu” kuliko kuwekeza katika
matibabu salama, yanayoaminika, yaliyofanyiwa utafiti na yanayoisaidia
dunia nzima. Matibabu ya hospitalini. Wengi wa waliodanganywa na
Loliondo, hasa wagonjwa wa Ukimwi, walishafariki dunia. Loliondo ilikuwa
ujanja mwingine na labda mradi wa wakubwa. Tunapenda sana mambo ya
mchezo kama Loliondo, huku tukikataa kuboresha sekta yetu ya Afya.
Viongozi hawaamini hospitali zetu, madaktari wetu na vifaa vyetu
Hii ni kasumba mbaya kuliko zote Afrika. Viongozi
wetu wengi hawaamini katika huduma zinazotolewa hapa nchini. Mara kadhaa
wamesafiri kwenda nchi za nje na kuona miundombinu ya sekta ya afya ya
nchi za wenzetu, wakiifananisha na hapa kwetu wanaona huku kwetu ni
“upuuzi” mtupu na hakuwezekaniki. Kwa sababu kiongozi ndiye njia, njia
inapoona mbele ni giza, maana yake mfuasi (mwananchi) hana cha
kubadilisha.
Tuna viongozi lukuki katika Serikali yetu
hawaamini kabisa kuwa sisi tuna hazina ya kutosha ya vijana ambao
tukiwaendeleza na kuwapa taaluma za kigeni na kisha tukawanunulia vifaa,
tukawapa mishahara mizuri, wakaishi katika nyumba nzuri na mazingira
rafiki kidogo tu, wanaweza kufanya hayo tunayoyafuata Marekani na Ulaya
kirahisi mno.
Ukishakuwa na Serikali ambayo haiwaamini askari
wake, silaha zao na hata ujasiri wao katika kuipigania nchi yao, je
utakuwa na jeshi linalofanya kazi kwa kujituma na kujiamini?
Haiwezekani. Vita ikitokea wakubwa wanaenda kukodi majeshi ya wazungu na
wakubwa wenzao waliondelea huko na kule ili kuwapigania, wakishaokolewa
wanasifia majeshi ya nchi hayo kwa kuwasaidia vita ambayo kama
tungejipanga, majeshi yetu yangepigana vita hiyo bila kukodi majeshi ya
nje.
Ndiyo maana sekta ya afya inazidi kudorora kila
uchwao, huku tukiwa tunaangalia. Ukienda vijijini, ndiko unaweza kulia,
kuna vijizahanati ambavyo havina msaada. Wauguzi wamekata tamaa na kuna
eneo lingine imeripotiwa hivi karibuni kwamba mlinzi alikuwa akihudumia
waja wazito kwa sababu hakuna nesi wa kufanya hivyo. Utakuta mtu
anakimbia hicho kijizahanati walau kwenda hospitali ya mkoa au wilaya,
huko nako kunakatisha tamaa.
Kituko cha “Uric Acid’
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment