Nani kahaba?

Unanicheka, ati ninauliza swali la kitoto sana kama siyo la kijinga, kwani kwa ufahamu wako, akili yako na hata kwa hali ya kawaida tu; unaamini ya kuwa kila mtu anajua ya kwamba ‘kahaba’ ni mwanamke basi!
Nasema hivyo kwani hata mimi mwenyewe niseme nilipoanza kuchipukiwa niliamini hivyo kuwa kahaba ni mwanamke; na wala sikusumbua akili yangu kutaka kujua ni mwanamke ki-vipi? Na kwa nini, na nililiona kuwa jina ‘kahaba’ ni dhahiri kwa wanawake.
Wapo wanajamii wanaokwenda mbali zaidi kifikra ya kwamba ‘makahaba’ ni baadhi ya wanawake wengi wanaoishi mjini; wengine huamini ya kuwa wasichana ambao hawajaolewa na wanafanya kazi mjini basi wote ni ‘makahaba’. Hii siyo kweli.
Dhana potofu
Kumekuwa na dhana potofu au kujengeka kwa uonaji wa kimoyomoyo bila yakuwa na uhakika ya kwamba binti yeyote “anapovunja ungo”, neno hilo hutumika kwa wasichana wanapo balehe, basi jambo lifuatalo ama haki ifuatayo kwao ni kuolewea tu.
Dhana hiyo imejengeka mno ndani ya jamii zetu miaka nenda-rudi hasa huko vijijini na imekuwa ikitekelezwa hivyo, pia baadhi ya makabila bila ya kuchelea ama niseme hakuna sumile kwa hilo.
Kutokana na dhana hiyo potofu baadhi hata niseme wasichana wengi wanapokosa kwa lugha ya kijijini “mtu wa kuwatokea”, yaani kupeleka barua ya posa hujiona kuwa hawana bahati au ni ‘mkosi’ kwao na kujijengea upweke wa maisha. Hali hiyo huweza kabisa kuwaletea kishawishi cha kuhamia mjini wakidhani huko wanaweza kupata bahati ya kuolewa kwa minajili ya kutojulikana na wanaume wa mjini juu ya makuzi yao ya awali.
Kahaba ni nani
Ni mtu wanaume au mwanamke anayeshiriki mambo ya uasherati kuwa ni biashara au starehe yake; malaya, mtembezi, mzinifu na mzinzi. Kwa maana hiyo basi hata wewe mwanaume unaesoma makala hii unaweza kuwa ‘kahaba’ ingawa wengi wanaliona hilo likiwaangukiwa baadhi ya wanaume wenye tabia au wanaofanya mambo ya ‘kike-kike’ almaarufu kama ‘mashoga’. Soma Biblia Mwanzo 19:1-29, uchafu wa miji ya Sodoma na Gomora, ukiwahusisha wanaume wenye tabia hizo, miji hiyo ilichomwa moto na Mwenyezi Mungu.
Kwa wanaume ‘starehe’ hiyo ya uzinifu kwa wengi wanaiona ni sifa ya kuwa rijali na wala hawaioni kuwa ni starehe chafu inayowaunganisha kwenye kundi hilo la ‘ukahaba’. Pia, hii nayo imejengwa kwenye dhana potofu ya kuwa wanaume ni viumbe wa viwango vya juu dhidi ya wanawake; na kuwachukulia wanawake kama ni ‘chombo’ cha starehe kwao, hivyo wao wanaume hawastahili kuitwa ‘makahaba’. Ni makahaba pia.
Uonevu wa dhati
Kutokana na hali ngumu ya maisha hasa kwa wanawake-madada, inayosababishwa na uonevu huu kuwa wao ni kiumbe cha daraja la pili, vipaumbele kwa mambo mengi ya kijamii yamelengwa kwa wanaume ingawa ni kimyakimya; sasa Serikali inapiga baragumu la usawa usiotimilizwa sawasawa.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post