Akikabidhi tuzo hiyo iliyotolewa na Umoja wa
Watendaji Wakuu (CEOrt) juzi, Balozi Ami Mbungwe alisema Rais Mkapa
ametoa mchango mkubwa katika kuimarisha utawala bora na uwazi ndani na
nje ya nchi.
“Alifanya kazi bila kuchoka, akisisitiza ukweli na
uwazi wakati wa kipindi cha kuboresho sera za uchumi. Atakumbukwa kwa
mchango wake mkubwa kwenye masuala ya uwekezaji,” alisema.
Akipokea tuzo hiyo katika hafla iliyohudhuriwa na
viongozi mbalimbali, Mkapa alisema ameipokea kwa niaba ya wananchi ambao
walikubali kupokea mabadiliko ya kiuchumi.
“Maono na mipango yangu wakati ule ilikuwa kuweka
mazingira rafiki ambayo yangelinda haki za sekta binafsi, kuhakikisha
mfumo wa fedha unakuwa rafiki kwa biashara, kukusanya mapato na kulipa
madeni ya umma ili kufan uchumi uwe imara,” alisema.
Mkapa alisema hata alipogundua kuwa ujasiriamali
unabanwa na kanuni zisizo sahihi, kodi kubwa, kukosekana kwa ushindani
halali, alihakikisha anaondoa vikwazo na kuongeza ushindani wa
kibiashara.
Alisema baadhi ya watu walilalamikia uboreshaji kwa madai kuwa sekta binafsi iligeuka sehemu ya kuficha kampuni za kigeni.
Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki alisema tuzo
hiyo mwaka jana ilitolewa kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali
Hassan Mwinyi, kutokana na mchango wake kwenye biashara huria, vyombo
vya habari na kuanzisha siasa za vyama vingi.
Mufuruki alisema nishani hiyo haitolewi tu kwa
viongozi wa kitaifa au marais, bali inakwenda kwa mtu yeyote ambaye
mchango wake unatambuliwa na jamii.
Alisema kiongozi huyo aliingia madarakani wakati
nchini ikiwa katika hali mbaya kiuchumi, lakini katika miaka miwili
aliteremsha mfumko wa bei kutoka asilimia 30 mpaka nne.
“Aliweza kusimamisha kuporomoka kwa thamani ya
shilingi, alihakikisha Serikali inatumia fedha ambayo inakusanya
kutokana na mapato yake ya ndani. alisema Mufuruki.
Katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu kutoka Ofisi ya
Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB), Omari Issa alipewa tuzo
ya Mwaka ya Utumishi wa Serikali kutokana na mchango wake alioutoa
kwenye sekta binafsi nchini.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment