Taarifa za kusambazwa kwa ripoti ‘feki’ ya IPTL jana ziliwagawa wabunge, baadhi wakitaka lijadiliwe huku Spika Makinda akipinga.
Tangu juzi, zimekuwapo taarifa za mtu mmoja
kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka akidaiwa
kuzisambaza zikiwa zimenyofolewa kurasa, zikidaiwa kuibwa katika Ofisi
ya Bunge, lakini polisi walipomhoji alisema alipewa na mbunge mmoja.
Hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe ilitolewa na
Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi akisema kuna umuhimu wa kujadili suala hilo na kutoa
maagizo ya kina kwa Serikali.
“Inavyoonekana taarifa hiyo imeibwa baada ya
kupokewa na Ofisi ya Bunge kwani katika ukurasa wake wa juu kuna muhuri
wa Bunge na inaonekana imepokewa Novemba 14 na Ofisi ya Katibu wa
Bunge,” alisema Mbatia.
Alisema kwa maelezo waliyopata ni kuwa taarifa
inayosambazwa imeibwa kabla ya kuwasilishwa PAC iliyopewa jukumu la
kuipitia na kupendekeza hatua za kuchukua.
“Baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwenye kamati
hiyo, kuna alama iliyowekwa kwenye nakala zote na katika taarifa
inayosambazwa alama hiyo haipo,” alisisitiza Mbatia.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (g) cha
Sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge, ni kosa kwa mtu yeyote
kusambaza waraka wowote ulioandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni
kabla ya wakati wake.
Alisema adhabu ya kosa hilo ni faini ya Sh500,000
au kifungo cha miaka mitatu jela na kuwa kitendo hicho kinalenga
kuliziba mdomo Bunge lisifanye kazi yake ipasavyo.
Baada ya kauli ya Mbatia, wabunge kadhaa walisimama kuonyesha kuiunga mkono, lakini Spika Makinda aliipinga.
Licha ya kumpongeza Mbatia na wenzake walioamua
kufuatilia taarifa za kusambazwa na nyaraka hizo na kutoa taarifa,
alisema anayehusika kuzisambaza ameshakamatwa na polisi, atashikiliwa
mpaka atakaposema taarifa anazozisambaza amezitoa wapi.
“Ndiyo kazi inayoendelea sasa, wamefikia mahali
(polisi) wanatumia ofisi yao kubwa ya Dar es Salaam kutambua mashine
zilizochapa hizo taarifa ni za nani. Kifungu cha 31 cha Kanuni za Bunge
kipo wazi, sasa tunajadili nini wakati mhusika yupo ndani?” alisema
Makinda.
Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge kuanza
kuzomea, lakini Spika Makinda alisisitiza kwamba suala hilo haliwezi
kujadiliwa bungeni.
- Soma zaidi Hapa(Mwananchi)
- Soma zaidi Hapa(Mwananchi)
Post a Comment