Mkosamali apandishwa kizimbani Kigoma

Kibondo. Mbunge wa Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, Felix Mkosamali amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo akikabiliwa na shtaka la kumzuia karani mwandikishaji kufanya kazi yake.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Peter Makala alidai jana mahakamani hapo kuwa mbunge huyo alitenda kosa hilo juzi, baada ya kufika Kituo cha Kitongoji cha Nduta, Kijiji cha Kumhasha, Kata ya Murungu, wilayani Kibondo na kumzuia karani kuendelea kuandikisha wakazi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Makala alidai kuwa kitendo cha kumzuia karani huyo kuendelea kufanya kazi yake ni kinyume na ukiukwaji wa Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Pia, alidai kuwa kitendo cha kuwazuia wakazi hao kujiandikisha ni kuwanyima haki yao ya msingi, kwani baada ya kuzuiwa waliendelea kudai kutaka kujiandikisha lakini mshtakiwa hakusikiliza kilio chao.
Mshtakiwa alikana shtaka na Hakimu Erick Marley alisema dhamana iko wazi kwa mdhamini kusaini bondi ya Sh4 milioni. Mbunge huyo alitimiza masharti na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29.
Mkosamali alikamatwa juzi jioni baada ya kudaiwa kumnyang’nya karani vitabu na madodoso na kuyapeleka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo.

Post a Comment

Previous Post Next Post