Raza amwakia waziri deni la Mapinduzi Cup

Aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masula ya michezo enzi za Dk Salmin Amour, Mohamed Raza.
Aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masula ya michezo enzi za Dk Salmin Amour, Mohamed Raza amewataka Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, naibu wake pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali Mwinyi kuwaomba radhi Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla kutokana na kuwadanganya.
Raza ametoa kauli hiyo kutokana na kukerwa na kauli tata za viongozi hao kuhusu deni lake analodai kuikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Desemba 27, 2013 kwa ajili ya kuandaa Kombe la Mapinduzi mapema Januari mwaka huu kupigwa danadana.

Akizungumza na NIPASHE juzi jijini Dar es Salaam, Raza ambaye ni mbunge na mfanyabiashara maarufu visiwani Zanzibar, alisema aliikopesha serikali ya Mapinduzi Zanzibar kiasi cha Sh. 71, 410,000 kwa makubaliano ya kulipwa mara baada ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, Januari 14, 2014 lakini hadi anazungumza na gazeti hili alikuwa hajalipwa hata senti moja.

Alisema licha ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Sherehe na Mapambo wa Mapinduzi Cup kuwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, huku akaunti aliyohamishia fedha hizo kutoka akaunti yake ikiwa ni ya serikali, amekuwa akizungushwa na kuelezwa kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hailitambui deni hilo.

Alisema Desemba 27, mwaka jana, Makamu  Mwenyekiti Mapinduzi Cup, Sharifa Khamis alifika ofisini kwake kutoa ombi la mkopo wa Sh. 71, 410,000 kwa ajili ya gharama za malazi na usafiri kwa awamu ya kwanza ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo.

Alisema kutokana na kutambua suala hilo ni la nchi, aliona ni lazima waipe heshima yake hivyo akaridhia kutoa mkopo huo bila riba lakini kwa makubaliano kwamba wakati wa marejesho alipwe kulingana na thamani ya shilingi kwa kutazama kwanza kiwango cha dola kilichopo sokoni.

"Wakati huo Sh. 71,410,00 ilikuwa ni sawa na dola 45,629 (Sh.1,565 kwa dola moja), hata hivyo, tulifuatana moja kwa moja na Sharifa kwenda benki kumkabidhi fedha hizo kwa vile walikuwa na akaunti ya Mapinduzi Cup kwenye Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), hivyo ilikuwa rahisi kuwahamishia kiasi hicho katika akaunti yao Na. 051108000099."

Alisema cha kushangaza Juni mwaka huu bungeni Zanzibar, waziri mwenye dhamana na michezo Zanzibar, Mbarouk alisema ndiyo kwanza analisikia na kwamba wizara yake kama imekopa milioni 70 hata siku moja haishindwi kulipa kiasi hicho.

"Mhe. Naibu Spika, mimi nilishakwenda kwa Mhe. Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Fedha nikataja shilingi bilioni 2, akaniambia subiri baada ya wiki mbili akanipa, iwe shilingi milioni 70," ilisomeka taarifa iliyotolewa bungeni wakati Raza alipoibua madai yake Juni mwaka huu.

Raza alisema aliendelea kujibiwa kuwa Mapinduzi Cup ni Taasisi isiyo ya Kiserikali (NGO) na kwamba si Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ilikopa fedha hizo, licha ya kupongezwa kwa juhudi zake za kufanikisha michuano hiyo na kuwakopesha.

Mbali na deni hilo, Raza ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini (CCM), alisema yeye pamoja na wafanyabiashara wengine waliombwa kuchangia kuanzia Sh. milioni tano ili kuwezesha michuano hiyo na kwamba kiasi hicho ndicho kilitegemewa kukusanywa kama sehemu ya kulipa madeni katika michuano hiyo.

"Mimi na wafanyabiashara wengine wengi tulichangia, hakika zilikuwa fedha nyingi huku tukiahidiwa tungepewa 'certificate' (vyeti) ambavyo vingetolewa na rais, lakini hilo halikufanyika na fedha nyingi zilichangwa. Sasa kama wameshindwa kunilipa si inamaana hata hizo tulizojitolea kuchangia zilitafunwa? Alihoji.

NIPASHE lilipomtafuta jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Mbarouk ili kuzungumzia madai hayo, hakupatikana kwa simu, hata hivyo lilimpigia Naibu Waziri wa wizara hiyo, Bihindu Khamis Hamad na lilipotaka kupata ufafanuzi huo, alisema: "Suala hilo anayeweza kulizungumzia ni katibu mkuu na waziri, watafute hao mimi siwezi kuongea chochote kile kwa sasa."

Hata hivyo, waziri mwenye dhamana ya michezo, alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi jana saa 10: 48, 11: 03 na 11:04 iliita bila kupokelewa na alipotafutwa tena baadaye hakupatikana kabisa. NIPASHE linaendelea kufanya jitihada za kuwatafuta wahusika hao ili kulizungumzia sakata hilo.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post