Mkude amshawishi Niyonzima atue Msimbazi

YANGA ilitaka kumsainisha Jonas Mkude ikachemka dakika za mwisho baada ya Simba kumshikisha kijana Sh70 milioni na kumboreshea maisha yake.
Sasa Simba nao wamemuweka kwenye rada yao kiungo wa Yanga anayemaliza mkataba wake, Hatuna Niyonzima.
Niyonzima ameeleza waziwazi kwamba hafurahishwi na jinsi kocha wa Yanga, Marcio Maximo anavyomtumia dakika chache na kutomueleza lolote kuhusiana na ufanisi wake hivyo hana mpango wa kuendelea na Yanga kama mambo yataenda kama yalivyo sasa.
Lakini Mkude baada ya kusikia Simba wanamtaka Niyonzima akawaambia: “Mtakuwa mna akili sana nyie, nileteeni jembe lile.”
Mkude ameiambia Mwanaspoti kwamba mchezaji huyo akitua Simba hali ya hewa itabadilika na kila mtu atanyamaza.
Mkude anaamini kwamba Niyonzima akitua Simba ataongeza ushindani zaidi kwenye safi ya kiungo kwa jinsi anavyomfahamu kwamba hana papara kwenye uamuzi wake uwanjani hivyo ni mtu sahihi kwa Mnyama. 
“Simba wakimsajili  Niyonzima watakuwa wamefanya jambo kubwa kwani ataongeza chachu ya ushindani mkubwa, hilo pia litatufanya sisi kuwa  mwiba kwa timu pinzani,kwa sababu ni mchezaji asiye na papara pia ana uwezo wa kucheza vema nafasi hiyo,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post