Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) ametaka
watu wote waliopokea fedha zaidi ya Sh73 bilioni kutoka kwenye akaunti
mbili za PAP katika Benki ya Stanbic iliyopokea fedha za escrow watajwe
majina na kufilisiwa mali zao.
Akichangia taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC) kuhusu sakata la fedha za escrow bungeni jana, alisema idadi ya
watu na kiwango cha fedha kilichochotwa ni kikubwa kuliko kilichokuwa
katika Benki ya Mkombozi.
Mnyika alisema anaunga mkono azimio namba tatu la
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), lililotaka watu wote waliogawiwa
fedha kutoka kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi kuzirudisha mara moja
na hata ikibidi kufilisiwa.
“Uchunguzi wa fedha za Stanbic usiishie tu kwa
watu waliochukua fedha, badala yake miamala yao ifuatiliwe ili ibainike
walikwenda kumlipa nani na wapi ili wachukuliwe hatua zinazostahili,”
alisema Mnyika.
Pia mbunge huyo alisema kuwa wakati fedha hizo
zikitolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri wa Fedha alikuwa anaumwa
na kwamba kumekuwapo na utata juu ya kifo cha waziri huyo.
“Wengine walihusisha kifo kile na masuala ya
utoaji wa fedha za escrow,” alisema Mnyika kabla Spika wa Bunge Anne
Makinda kusimama na kumtaka asimtaje waziri huyo.
“Naomba nikumbushe, mwenye mzazi wake aliwaombeni
msimshirikishe baba yake katika maneno haya, naombeni sana mnaumiza
familia za watu bila sababu,” alisema Makinda.
Hata hivyo, Mnyika alimpa pole mtoto huyo na
kusema kuwa kwa kulitambua hilo, ndiyo maana hakumtaja mtu bali alikuwa
akizungumzia cheo cha aliyekuwa waziri wa fedha wakati huo.
“Nazungumzia nafasi ya Waziri wa Fedha katika
mchakato mzima, nani alikuwa anakaimu nafasi ile kipindi kile, nini
kilitokea wakati ule Bunge linahitaji kuelezwa,” alisema Mnyika.
Vilevile alisema kwa kuwa Serikali inaona
kigugumizi kumwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutokana na kushindwa
kuisimamia Serikali, Bunge litamwajibisha kwa kuandaa saini za kutokuwa
na imani naye.
Mdee
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema
kauli ya Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuwa kuna fedha za kodi
ziliibiwa, ina maanisha kuwa hasara hiyo ni matokeo ya ushauri
uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment