Dar. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven
Wassira amewataka wote wanaotumia suala la ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu ya Serikali (PAC) kwa vigezo vya kuwaondoa wenzao katika mbio za
urais hawastahili kupewa nafasi hiyo.
“Wanaotaka urais kama wapo (ni pamoja na mimi)
ambao wanaona mbinu ni kuwaondoa wengine kwa nguvu, hao hawafai kupewa
urais wa nchi hii. Urais ni lazima ushindaniwe kwa haki na vyama vyote
vipewe nafasi ya kushiriki. Kama unataka urais ushindani uwe kwa njia
sahihi,” alisema.
Alisema ni bora kuwa maskini anayeheshimika kuliko
kukubali kuwa tajiri anayedharauliwa na kutukanwa kutokana na mapato
yasiyokuwa halali.
Wassira alieleza kwamba kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwamba baadhi ya watu walikwenda
kuchukua fedha wakiwa na magunia, mifuko ya sandarusi, rumbesa na
maboksi katika moja ya benki, ni vyema uchunguzi ukifanyika ili
kuwatambua watu hao na hatua zaidi zichukuliwe.
“Ni lazima tufuatilie na vyombo vyetu vya sheria
vituambie ni kina nani hao, vinginevyo hatuna nchi. Tukubali hawa watu
wabebe mizigo yao, hakuna CCM ya wezi, ila kuna wezi ndani ya CCM, hivyo
wezi ni lazima wabebe mizigo yao,” alisema.
Alisisitiza kwamba ripoti hiyo ya PAC inatakiwa
kuheshimiwa na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuihoji uhalali wake
kwa kuwa inatokana na kamati maalumu inayotambuliwa na Bunge
iliyokusanya taarifa kutoka kwa vyombo vinavyoaminika vya Serikali,
ambavyo ni Takukuru na CAG.
Profesa Mwandosya
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi maalumu,
Profesa Mark Mwandosya alisema Serikali ni lazima ijifunze kutokana na
kashfa hii kwa kuwa inaonekana kabisa wapo watu wasiowajibika sawasawa
katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema ni vyema kuangalia upya sheria zilizopo na
ikibainika maeneo ambayo yanatoa mwanya wa kuwapo udhaifu zirejeshwe
bungeni na zifanyiwe mabadiliko ili kuondoa udhaifu uliopo.
Mwandosya alivitaka vyombo vya sheria vifanyie
kazi maazimio yaliyofikiwa katika Bunge hilo jana na vifanye kazi kwa
haraka, uadilifu na uhuru ili kutoa majibu mapema kwa Watanzania.
Alisisitiza kwamba Kamati ya PAC imefanya kazi
kubwa na kwamba hakuna anayeweza kupinga kwamba fedha za Escrow ni za
umma kwa kuwa dhamana yake imebebwa na Benki Kuu ambayo Gavana wake
anawajibika kutunza fedha za umma
- Mwananchi
Post a Comment