Wassira acharukia wataka urais

Dar. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira amewataka wote wanaotumia suala la ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Serikali (PAC) kwa vigezo vya kuwaondoa wenzao katika mbio za urais hawastahili kupewa nafasi hiyo.
“Wanaotaka urais kama wapo (ni pamoja na mimi) ambao wanaona mbinu ni kuwaondoa wengine kwa nguvu, hao hawafai kupewa urais wa nchi hii. Urais ni lazima ushindaniwe kwa haki na vyama vyote vipewe nafasi ya kushiriki. Kama unataka urais ushindani uwe kwa njia sahihi,” alisema.
Alisema ni bora kuwa maskini anayeheshimika kuliko kukubali kuwa tajiri anayedharauliwa na kutukanwa kutokana na mapato yasiyokuwa halali.
Wassira alieleza kwamba kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwamba baadhi ya watu walikwenda kuchukua fedha wakiwa na magunia, mifuko ya sandarusi, rumbesa na maboksi katika moja ya benki, ni vyema uchunguzi ukifanyika ili kuwatambua watu hao na hatua zaidi zichukuliwe.
“Ni lazima tufuatilie na vyombo vyetu vya sheria vituambie ni kina nani hao, vinginevyo hatuna nchi. Tukubali hawa watu wabebe mizigo yao, hakuna CCM ya wezi, ila kuna wezi ndani ya CCM, hivyo wezi ni lazima wabebe mizigo yao,” alisema.
Alisisitiza kwamba ripoti hiyo ya PAC inatakiwa kuheshimiwa na kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuihoji uhalali wake kwa kuwa inatokana na kamati maalumu inayotambuliwa na Bunge iliyokusanya taarifa kutoka kwa vyombo vinavyoaminika vya Serikali, ambavyo ni Takukuru na CAG.
Profesa Mwandosya
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi maalumu, Profesa Mark Mwandosya alisema Serikali ni lazima ijifunze kutokana na kashfa hii kwa kuwa inaonekana kabisa wapo watu wasiowajibika sawasawa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema ni vyema kuangalia upya sheria zilizopo na ikibainika maeneo ambayo yanatoa mwanya wa kuwapo udhaifu zirejeshwe bungeni na zifanyiwe mabadiliko ili kuondoa udhaifu uliopo.
Mwandosya alivitaka vyombo vya sheria vifanyie kazi maazimio yaliyofikiwa katika Bunge hilo jana na vifanye kazi kwa haraka, uadilifu na uhuru ili kutoa majibu mapema kwa Watanzania.
Alisisitiza kwamba Kamati ya PAC imefanya kazi kubwa na kwamba hakuna anayeweza kupinga kwamba fedha za Escrow ni za umma kwa kuwa dhamana yake imebebwa na Benki Kuu ambayo Gavana wake anawajibika kutunza fedha za umma
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم