Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),John Mnyika.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema hayo jana alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha Kamati ya Utendaji la Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), kinachofanyika mjini hapa.
Alisema iwapo vijana watakubali katiba hiyo kupita, watakuwa wameruhusu ufisadi kupita na hivyo, kuchangia kurudisha nyuma maendeleo nchini.
Pia aliwataka vijana kuhakikisha wanapata baraza la vijana la taifa ili walitumie kujadiliana masuala yanayowahusu, kwani jamii ya Watanzania ina imani nao.
Alisema vijana wameanza kudai muswada wa kuunda baraza hilo tangu mwaka 1996 wakitaka ujadiliwe bungeni, lakini Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiupinga kutokana na kuhisi kwamba, unaweza kuua Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM).
Mnyika alisema Watanzania wamekuwa na imani na vijana, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanakidhi haja yao kwa kupambana ili wawe na umoja wao, ambao utawasaidia kujadiliana baadhi ya mambo yanayohusu umoja huo.
“Watanzania wana imani na vijana, lakini tatizo ni CCM, wamekuwa wakiona kukiwa na umoja wa taifa wa vijana, umoja wao utakuwa umekufa.Sasa hili tulipigie kelele kwa nguvu zote,” alisema Mnyika.
Aliongeza: “Jambo hili mnatakiwa mlijadili katika kikao chenu, kwani kumbukeni nyie ni vijana, hamuwezi kuwa vijana maisha yenu yote. Sasa hivi nina miaka 34. Mwaka kesho siyo tena kijana, kwa sababu nitakuwa na miaka 35. Ndiyo maana nawasihi mlipiganie hili.”
Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita, alisema lengo la mkutano huo ni kuwapa darasa viongozi wapya wa baraza hilo waliochaguliwa ili kupambana na CCM.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment