Yanga imchunguze Maximo kabla ya kumsajili Emerson

Katuni
Klabu ya Yanga imetangaza rasmi kuwa kesho inatarajia kumpokea kiungo Mbrazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe kufanya majaribio na baadaye vipimo vya afya na kama atafuzu, basi watamsajili katika usajili huu wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15 kabla ya kufungwa Desemba 15, mwaka huu.
Emerson (24), ambaye inaelezwa kuwa anatokea klabu ya Bonsucesso FC  inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Brazil, msimu uliopita, pia aliichezea Piotrkow Trybunalski ya daraja hilo ya nchini Poland.

Yanga imeeleza kutua kwa Emerson kunatoka na mshambuliaji Geilson Santos Santana “Jaja” kuwataarifu kuwa hatarejea tena nchini kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia, hivyo inataka nafasi hiyo izibwe na Mbrazil mwenzake huyo.

Kwanza kabisa, tunaipongeza Yanga kwa kuleta wachezaji kutoka Brazil, nchi ambayo imepiga hatua kubwa kisoka duniani, jambo ambalo litaongeza ufundi, juhudi na hata hamasa kwa wachezaji wetu wa ndani.

Tunaamini Yanga inaweza kuwa klabu pekee ama inayoongoza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa kuwa na wachezaji kutoka Brazil, hivyo kuzifanya nchi nyingi duniani kuwa na shauku ya kuitupia macho Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pamoja na pongezi hizo, awali wakati Jaja na mchezaji mwenza kutoka Brazil kiungo Andrey Coutinho walipowasili na kuanza kusifiwa kwa umahiri wao mazoezini, kupitia vyombo mbalimbali vya habari si  NIPASHE, gazeti hili lilikuwa la kwanza kueleza ni vema mashabiki, viongozi na wote wenye mapenzi mema na Yanga wakasubiri kumuona Jaja na Coutinho katika ligi ndipo wasifiwe kwa sababu hicho ndicho kipimo halisi cha mchezaji.

Tulieleza kwa mapana kwamba kipimo halisi cha mchezaji ni uwanjani katika mechi za kimashindano na si katika mazoezi ama mechi za kirafiki ambazo hata hivyo hawakuwahi kuonekana wakicheza hapo kabla.

Hata hivyo, ni mechi saba tu za Ligi Kuu Bara zimedhihirisha kile tulichokuwa tumekieleza baada ya Yanga kubaini kuwa uwezo wa Jaja ni mdogo kuliko hata wachezaji wetu wa ndani, ingawa klabu hiyo haikuwa tayari kueleza kuwa imemtema kutokana na kiwango duni.

Hilo linatupa hofu tena kutokana na ujio wa Mbrazil mwingine, Emerson katika kikosi hicho hasa kutokana na ukweli kwamba ni Kocha Mkuu, Marcio Maximo yuleyule aliyependekeza Jaja asajiliwe kwa kuwa alikuwa akikifahamu vema kiwango chake, na sasa amekuja tena na pendekezo la kiungo huyo.

Yanga inapaswa kumhoji ama kumuuliza Maximo maswali magumu kabla hata ya kumsajili kwani tunaamini si rahisi Emerson akashindwa kufuzu majaribio kwa sababu anayempima na kutoa mapendekezo asajiliwe ama la, ni Maximo ambaye amemleta na anayetamani kumuona akiichezea klabu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani.

Kwa ushauri nafuu, NIPASHE tunaishauri Yanga kuunda jopo la makocha wakiwamo wazawa ambao watachunguza uwezo wa Emerson na kutoa maoni yao kabla ya Mbrazil huyo hajamwaga wino.

Tunaamini kiasi cha fedha ambacho Yanga itakitumia kulipa jopo hilo la makocha kinaweza kuwa mshahara wa mwezi mmoja tu wa Emerson atakaolipwa endapo atasajiliwa na Yanga.

Mfano mzuri ni kama Yanga ingetumia utaratibu kama huu tunaoupendekeza, ungekuwa imeokoa mamilioni ya fedha ambazo imezitumia kumlipa Jaja ambaye baadhi ya mashabiki, wanachama na hata viongozi walikuwa wakidai ni 'mzigo' kwa klabu kwa kuwa hana msaada ukilinganisha na wazama kama Jerry Tegete ambaye walidai alikuwa akibaniwa nafasi na kocha ili kumbeba Mbrazil mwenzake.

NIPASHE tunaamini wageni wanaongeza changamoto kubwa kwa wazawa na wanaboresha ligi yetu, lakini baadhi ya wachezaji wakigeni ambao wanasajiliwa na klabu zetu wanakuja kuvuna fedha tu na kuwanyima nafasi wazawa ya kukuza vipaji vyao. Kuna haja kubwa viongozi wa klabu kuwa makini na aina ya wachezaji wa nje wanaowasajili ili kulinda vipaji vya ndani na hilo linapaswa kutazamwa kwa kina pia na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwani ndilo linalobeba dhamana yote ya soka la Tanzania.

TFF isikubali Ligi Kuu ya Tanzania Bara kugeuzwa sehemu ya wageni kuja 'kupiga pesa' na kuiacha ikiendelea kuporomoka na kupoteza mvuto jambo ambalo kwa kiasi kikubwa pia litaporomosha hata timu yetu ya Taifa, Taifa Stars.

Tunatambua wazi ongezeko la wageni wenye vipaji vikubwa katika soka litawaimarisha wazama na hivyo kuwafanya kuwa msaada kwa Stars.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post