Mshirika wa Waziri Muhongo anaswa na ripoti feki ya CAG


Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime 

JESHI la Polisi mkoani hapa, linamshikilia mtu mmoja kwa madai ya kukutwa na ripoti  ya kughushi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti hiyo ambayo ni matokeo ya uchunguzi wa CAG kuhusu kashfa ya kuchota fedha kwenye Akaunti ya Escrow, imenyofolewa kurasa tano muhimu ambazo zinaonyesha namna fedha hizo zaidi ya sh bilioni 300 zilivyochotwa na jinsi watuhumiwa walivyohusika.
Ingawa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime hakumtaja jina, lakini Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bara, John Mnyika amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Mohamed Mbarouk, ambaye alikutwa na nyaraka hizo juzi usiku katika Hoteli ya Dodoma.
Mbarouk anaelezwa kuwa ni rafiki na mtu wa karibu sana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, alikiri kumshikilia mtu huyo pamoja na nyaraka alizokutwa nazo.
Alisema nyaraka hizo zimeibwa kutoka ofisi ya Katibu wa Bunge na zina muhuri wa siri wa ofisi hiyo.
Alisema ripoti hiyo feki, imenyofolewa kurasa tatu, 57, 58 na 59 ambazo zinatoa maelezo muhimu kuhusu uchunguzi wa kashfa hiyo ya Akaunti ya Escrow.
Ripoti hiyo imesambazwa mitaani na inadaiwa inapotosha ukweli kuhusu kashfa hiyo.
Akizungumza na Gazeti hili, Mnyika alisema aliyekamatwa ni Mbarouk Mohammed ambaye ana uhusiano wa karibu na Profesa Muhongo.
Alisema wanalitaka jeshi la Polisi kufanya uchunguzi haraka wa tukio hilo ili kujua waliohusika na uhalifu huo.
- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post