
Mshambuliaji mahiri wa Yanga na timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars),Simon Msuva.
Msuva ametajwa kuwa na mipango ya kutaka kuhamia Simba hali iliyosababisha Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Wekundu wa Msimbazi, Zacharia Hanspoppe, kutangaza hadharani kwamba wanapeleka barua rasmi Yanga ya kutaka kumsajili winga huyo na kutamka kwamba wanataka 'kumrejesha' nyumbani.
Akizungumza na NIPASHE jana, Msuva, alisema licha ya kuwa na mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuichezea Yanga, klabu hiyo na watani zao Simba zote ni majanga na kwamba kwake ni za kupita tu ila kwa sasa hana budi kuheshimu mkataba huo wa alioingia rasmi kisheria na klabu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.
Msuva alisema kuwa kauli za yeye kutakiwa Simba na kudaiwa kwamba ana mapenzi na klabu hiyo vinamuumiza kwa sababu klabu hizo ni pinzani na yeye soka ndiyo kazi anayoitegemea.
Alisema hajawahi kufanya mazungumzo na kiongozi yoyote wa Simba kwa sababu anafahamu vipengele vilivyoko kwenye mkataba wake haviruhusu kufanya hivyo.
"Mimi ni mchezaji wa Yanga, nina mkataba na sijawahi kuzungumza na viongozi wa Simba, hata huyo Hanspoppe hajawahi kunipigia simu, inaniumiza na inanichanganya sana, nafikiria kuitumikia vyema kwenye mechi za ligi na mashindano ya kimataifa tutakayoshiriki mwakani," alisema winga huyo.
Aliongeza kuwa Simba kama wanamuhitaji wanatakiwa kuwa na subra hadi mkataba wake utakapomalizika ndipo wafuate taratibu husika na si kuzungumza maneno ambayo yanaweza kumharibia.
"Mimi ni mchezaji, ninaweza kuhama, lakini kwa sasa nguvu zangu zote naelekeza kuitumikia Yanga, siwezi kwenda kinyume, pia bado sijafika, nafikiria kupata timu hata nje ya nchi," aliongeza.
Uongozi wa Yanga ulimpa Msuva pamoja na nyota wengine kadhaa wa kikosi cha kwanza mkataba mpya wa miaka miwili baada ya kuona kiungo wao, Frank Domayo ametua Azam.
Yanga ambao mwakani wataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho inadaiwa kutaja thamani ya Msuva sasa ni Sh. milioni 300.
Hata hivyo, habari kutoka Simba zinaeleza kuwa tayari wameshaanza kujipanga kukusanya fedha ili kumnasa nyota huyo na kiongozi mmoja wao ameahidi kutoa peke yake Dola za Marekani 40,000.
Kipindi cha dirisha dogo kimefunguliwa na kinatarajiwa kumalizika Desemba 15, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment